UN na sekta ya michezo kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi:COP24

Mchezaji wa soka wa Canada, Karina LeBlanc katika uzinduzi wa mezindua mfumo wa kuyakusanya mashirika ya michezo,kuchagiza kufikia malengo ya mkataba wa Paris.  .
UNFCCC/James Dowson
Mchezaji wa soka wa Canada, Karina LeBlanc katika uzinduzi wa mezindua mfumo wa kuyakusanya mashirika ya michezo,kuchagiza kufikia malengo ya mkataba wa Paris. .

UN na sekta ya michezo kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi:COP24

Masuala ya UM

Sekta ya michezo na kitengo cha Umoja wa Mataifa cha kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi leo wamezindua mfumo wa kuyakusanya mashirika ya michezo, timu, wanamichezo na mashabiki kwatika juhudi za pamoja za kuchagiza na kuchukua hatua ili kufikia malengo ya mkataba wa Paris .

Wawakilishi kutoka sekta pana ya michezo duniani walishirikiana kwa karibu na kitengo cha mabadiliko ya tabia nchi cha Umoja wa Mataifa mwaka jana wameunda mfumo huo ili kupunguza kiwango cha utoaji wa hewa chafuzi katika operesheni za michezo na kutumia mwanya wa umaarufu na hamasa ya michezo kushirikisha mamilioni ya mashabiki katika juhudi hizo.

Mfumo huo uliozinduliwa leo una malengo makuu mawili , mosi ni kufikia azma ya wazi kwa jamii ya kimataifa ya michezo ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi  , na kutumia michezo kama nyenzo ya unganishi katika kuchagiza kampeni na hatua dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi miongoni mwa raia wa kimataifa.

Uzinduzi huo uliofanyika kandoni mwa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi COP24 mjini Katowice Poland, ulijumuisha wadau waanzilishi ikiwemo kamati ya kimataifa ya michezo ya Olimpiki (IOC) Shirikisho la soka duniani (FIFA), shirikisho la kimataifa la wapiga makasia, klabu ya mpira wa miguu ya Forest Green Rovers na shirikisho la tenesi la Ufaransa Roland Garros), waandaaji wa Tokyo Olimpiki ya 2020 na Paris Olimpiki 2024.

 

wakimbizi vijana  wakiwa nchini Marekani hujifariji kwa mchezo wa soka.
IOM 2018/Ahmed Badr
wakimbizi vijana wakiwa nchini Marekani hujifariji kwa mchezo wa soka.

Akizumgumzia mfumo huo mwenyekiti wa tume endelevu ya IOC Prince Albery II amesema “Kwa uwezo wake wa kufika mbali, ushawushi wake duniani kote na uwezo wake wa kuchagiza na kushawishi mamilioni ya watu kote duniani , michezo inafursa ya kipekee kusongesha mbele hatua za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuchagiza wafuasi kujiunga katika kampeni na tuko tayari kutumia fursa ya michezo kuunga mkono juhudi hizi.”

Nao viongozi na wawakilishi wa mashirika na vyombo vingine vya michezo waliohudhuria uzinduzi huo wamesema ahadi yao ya kulinda dunia dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi iko palepale na watatumia kila uwezo wao kushawishi dunia na hususan mashambiki wa michezo umuhimu wa ajenda hii.

Sekta ya michezo inachangia uchafuzi wa mazingira kwa njia nyingi ikiwemo usafiri, matumizi ya nishati, ujenzi wa viwanja, mapishi, na njia zingine na imekubali kuwajibika kupunguza gesi ya viwandani sanjari na matakwa ya mkataba wa Paris.