Madagascar, Uganda na Zambia ziko tayari kufaidika na fursa za uchumi wa kidijitali.

10 Disemba 2018

Tathimini  iliyochapishwa na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo UNCTAD kuhusu utayari wa biashara mtandaoni, imeonesha mitandao ya simu inachochea biashara za mtandaoni katika nchi za Madagascar, Uganda na Zambia.

Kwa msingi huo hali hiyo inaziweka nchi hizo katika nafasi nzuri ya uchumi wa kidijitali na hivyo kusongesha biashara katika nchi hizo tatu umebaini.

Ripoti tatu ambazo zinaonesha utayari katika maeneo saba ya sera chini ya mwongozo wa UNCTAD wa biashara kwa wote, zimezinduliwa leo mjini Nairobi Kenya katika siku ya ufunguzi wa wiki ya kujadili biashara mtandaoni barani Afrika.

Akiizungumzia ripoti hiyo, Katibu mkuu wa UNCTAD Mukhisa Kituyi amesema mapendekezo katika ripoti hizo yanaweka msingi wa wadau wa biashara mtandaoni, “faida za mapendekezo hatutaweza kuzihisi kama hazitatekelezwa ipasavyo. Hii itahitaji kujumuisha mapendekezo katika mipango ya maendeleo ya taifa, Serikali, sekta binafsi, sera za teknolojia ya mawasiliano, mipango ya kisheria na miradi ya maendeleo”.

Ripoti imeongeza kuwa hivi sasa biashara mtandaoni na ujasiriamali wa kidijitali unazidi kuongezeka barani Afrika wakitaja kuwa zaidi ya wakazi wa Afrika milioni 21 wananunua bidhaa mtandaoni ijapokuwa nchi ziko katika ngazi mbalimbali za kimaendeleo. 

Malipo ya miamala kwa njia ya kidijitali yanatumika sasa kuinua uchumi wa nchi mbalimbali duniani ikiwemo Afrika
Benki ya Duniak/Simone D. McCourtie
Malipo ya miamala kwa njia ya kidijitali yanatumika sasa kuinua uchumi wa nchi mbalimbali duniani ikiwemo Afrika

Mathalani nchini Uganda, matumizi ya simu katika masuala ya fedha yamefikia bilioni 16.3 sawa na nusu ya pato la nchi. Lakini huko Zambia ambako kumekuwa na mdororo kiasi kwani bado watu wanapenda kufanya malipo kwa fedha halisi baada ya mzigo kufika. 

Madagascar ni asilimia 6 tu ya watu wote wanaotumia intaneti na ni asilimia 4 tu wana akaunti ya benki lakini hiyo inamaanisha kuwa wauzaji wanaweza kukubali kupokea malipo ya mtandaoni kwa njia ya simu. 

Nchi zote tatu yaani Uganda, Madagascar na Zambia wamepokea tathmini hiyo mpya ambapo Waziri wa nchi anayehusika na ushirika nchini Uganda Frederick Gume Ngobe amesema, “biashara mtandaoni ni msukumo kwa ujasiriamali, ubunifu na maendeleo ya biashara ambayo yanaweza kuwanufaisha waganda wote”

Naye Katibu mkuu wa Wizara ya biashara Zambia Bi Kayula Siame akasema ripoti hii inatoa ramani kwa ajili ya sera za Zambia na hivyo inawaonesha kile wanachotakiwa kukifanya.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter