Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Posta yazinduka sasa nchi 9 kuanza mchakato wa kutoa huduma za kifedha

Kwa takwimu za miaka ya hivi karibuni, posta husafirisha barua bilioni 368.4 na vifurushi bilioni 6.4 kila mwaka.
Photo: Universal Postal Union (UPU)
Kwa takwimu za miaka ya hivi karibuni, posta husafirisha barua bilioni 368.4 na vifurushi bilioni 6.4 kila mwaka.

Posta yazinduka sasa nchi 9 kuanza mchakato wa kutoa huduma za kifedha

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la posta duniani, UPU leo limetangaza mataifa 9 ambayo mashirika yake ya posta yataanza kunufaika na pogramu yake ya kusongesha huduma za kifedha kidijitali kwa njia ya posta.

Akizungumza mjini Nairobi, Kenya wakati wa mada ya kuchagiza ujumuisha wa fedha kupitia huduma za fedha kwa njia ya simu za kiganjani, kwenye mkutano wa jinsi ya kuchagiza biashara mtandao barani Afrika,  Mkurugenzi Mkuu wa UPU Bishar A. Hussein ametaja nchi hizo kuwa ni  Benin, Côte d’Ivoire, Ghana, Kiribati, Nauru, Pakistan, Rwanda, Tonga na Vietnam.

Bwana Hussein amesema, “kuchukua hatua thabiti kwa kuendeleza miamala ya fedha kwa njia ya simu za mkononi kupitia huduma za posta huko mashinani, kutasaidia ni manufaa kwa jamii ambazo bado hazijafikiwa na huduma hizo pamoja na sekta za biashara.”

Amesema kuwa hivi sasa wanajenga ubia na wahisani wa kimataifa na sekta binafsi ili kusaidia mashirika ya posta kwenye safari yao hiyo ya kuweka mifumo ya kidijitali ya kuweza kufanya miamala ya fedha.

Mkurugenzi Mkuu wa UPU Bishar A. Hussein
UPU
Mkurugenzi Mkuu wa UPU Bishar A. Hussein

 

Kupitia FITAF, ambao ni mradi wa kiufundi wa kusaidia UPU kusongesha huduma za kifedha kidijitali,huduma za posta kwenye nchi husika zitajengewa uwezo ili huduma za fedha kidijitali ziweze kufikia mtu kwa usalama popote alipo, wakati wowote na hivyo kuwezesha biashara ndogo ndogo kupata ufadhili wa kifedha wanaohitaji ili kuchangia kwenye uchumi wa nchi yao.

Miradi itawezesha mashirika manne ya posta kuanzisha mifumo ya kuwezesha kufanyika malipo  ya miamala kwa njia ya simu pamoja na huduma za kutunza fedha na bima, ilhali mashirika matano yatajengewa uwezo wa kuelewa na kuchunguza fursa za masuala ya fedha kwa mfumo wa kidijitali.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, watu wazima bilioni 1.7 duniani hawajafikiwa na huduma rasmi za kifedha ambapo bilioni moja kati yao ni wanawake. “Kukiwa na vituo zaidi ya 670,000vya posta  vinavyofikia maeneo ya ndani zaidi duniani, posta ndio mdau bora zaidi wa kufikisha huduma za ujumuishaji wa kifedha,” amesema Bwana Hussein.

UPU yenye makao yake makuu huko Berne, mji mkuu wa Uswisi, ilianzishwa mwaka 1874 na ni moja ya mashirika ya zamani zaidi duniani na jukumu lake kuu ni kuimarisha ushirikiano baina ya wadau wa posta.

Mkutano wa wiki moja wa biashara mtandao barani Afrika huko Nairobi, Kenya umeadaliwa na kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.