Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

SafeBoda yawainua kiuchumi wachuuzi na waendesha bodaboda Uganda

Sokoni mjini Kampala Uganda
World Bank/Arne Hoel
Sokoni mjini Kampala Uganda

SafeBoda yawainua kiuchumi wachuuzi na waendesha bodaboda Uganda

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Uganda, apu ya kuunganisha wachuuzi wa bidhaa sokoni na wateja wao imekuwa na msaada mkubwa kwa kijana David Akanshumbusha wakati huu ambapo nchi hiyo iko kwenye kizuizi cha kuchangamana kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Akanshumbusha ambaye ana genge la kuuza bidhaa katika soko la Nakawa lililoko mji mkuu wa Uganda, Kampala ni mwanachama pia wa SafeBoda, ambayo ni apu ya kusaidia waendesha bodaboda kupata wateja, apu ambayo sasa pia inatumika kuunganisha wachuuzi wa sokoni na wateja.

Wateja wanaandika mahitaji yao ya bidha akupitia SafeBoda na kulipa kwa njia ya simu za rununu na kisha waendesha bodaboda walioko sokoni Nakawa wanapelekea wateja bidhaa hizo kwa bodaboda.

“Nashukuru sana apu hii, hivi sasa nina wateja wengi zaidi kuliko ilivyokuwa awali,”  anasema  Akanshumbusha.

Apu hiyo imeboreshwa na kuwezeshwa kutumika kufanyia biashara ya mtandao na hivyo kuongeza mauzo ya mfanyabiashara huyo na wengine wengi ambao sasa wananufaika na mauzo ya biadhaa zao kutoka maelfu ya wateja.

Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, inasema kuwa majukwaa au apu za biashara mtandao kama vile SafeBoda yanasaidia kulegeza hali ngumu ya uchumi itokanayo na COVID-19.

UNCTAD inasema kuwa hivi sasa serikali ya Uganda inasidia kuimarisha majukwa hayo na kuweka mazingira bora ya biashara mtandao na uchumi wa kidijitali kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotokana na tathmini ya UNCTAD juu ya utayari wa Uganda kwenye biashara mtandao.