Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Paza sauti kutetea haki za binadamu- kilele ni leo!

Watoto katika moja ya matukio maalum ya maadhimisho ya miaka 70 ya tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, UDHR
UN /Mark Garten
Watoto katika moja ya matukio maalum ya maadhimisho ya miaka 70 ya tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, UDHR

Paza sauti kutetea haki za binadamu- kilele ni leo!

Haki za binadamu

Leo ni siku ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni tarehe ya kukumbuka kupitishwa kwa azimio la haki za binadamu duniani, UDHR ambalo leo linatimiza miaka 70.
 

Azimio hilo lilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 10 mwezi desemba mwaka 1948 huko Paris mji mkuu wa Ufaransa. 

Likipatiwa jina la tamko la haki za binadamu, nyaraka hiyo inaweka viwango vya pamoja vya haki za binadamu kwa wote na mataifa yote. 

Azimio hilo, kwa mara ya kwanza liliweka misingi ya haki za binadamu inayokubalika kimataifa na inayopaswa kulindwa popote pale duniani. Hadi sasa nyaraka hiyo imetafsiriwa kwa zaidi ya lugha 500 ikiwemo Kiswahili.

 Wanawake kutoka Japan wakitizama tamko la haki za binadamu walipotembelea makao makuu ya muda ya Umoja wa Mataifa Feb 1950 yaliyokuwa Lake Success, New York Marekani.
UN Photo.
Wanawake kutoka Japan wakitizama tamko la haki za binadamu walipotembelea makao makuu ya muda ya Umoja wa Mataifa Feb 1950 yaliyokuwa Lake Success, New York Marekani.

Maadhimisho haya yanaambatana na shughuli mbalimbali kuanzia Suva barani Asia hadi Johannesburg, Mexico hadi Los Angeles,kwa lengo la kuendeleza, kushirikisha na kutathmini Azimio hilo na umuhimu wake katika maisha ya kila siku.

Shughuli za leo ni kilele cha harakati zilizoanza mwezi desemba mwaka jana.

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New  York, Marekani kutakuwepo na mjadala kuhusu umuhimu wa tamko hilo, ilhali “tuzo kwa washindi wa tuzo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka huu wa 2018 itatolewa tarehe 18 mwezi huu,” imesema ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Huko Geneva, Uswisi kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa kunafanyika shindano la Haki zangu ndani ya sekunde 180 ambako watoto walitakiwa kutuma video ya sekunde 180 ikifafanua haki zao.

UN News
Miaka 70 ya UDHR

Mbinu mbalimbali zimetumika kufafanua yaliyomo kwenye tamko hilo ikiwemo uchambuzi wa ibara kwa ibara, sambamba na video inayoonyesha baadhi ya watu akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakitaja haki zilizomo kwenye tamko hilo kwa lugha nane, ambazo ni kiswahili, kireno, kiarabu, kispanyola, kachina, kirusi, kifaransa na kiingereza.

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Michelle Bachelet kupitia ujumbe wake wa siku ya leo amesema “tamko hili lililopitishwa baada ya vita vikuu vya pili vya dunia limekuwa mwongozo wa kusimamia haki na ulinzi wa kijamii, kupatia watu fursa za kiuchumi na ushiriki kwenye siasa.” 

Amesema popote pale ambapo azimio hilo lenye ibara 30 limeheshimiwa, utu wa mamilioni ya watu umeinuliwa na machungu yameepushwa.

Bi. Bachelet amesema “katika zama za sasa za misukosuko, tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ni mbinu sahihi ya kutuongoza.”