Haki za binadamu ni chombo cha kumuendeleza mwanadamu: Guterres

Kauli ya kuwa masuala ya haki za binadamu duniani yamepitwa na wakati na badala yake utaifa ndio kitu muhimu kinachopashwa kupewa msisitizo imepingwa na baadhi ya viongozi ambao wanakutana mjini New York Marekani kuzindua jukwaa lililopatiwa jina “habari njema za haki za binadamu.”
Akizungumza kwenye uzinduzi huo Bi Federica Moghrini, makamu rais wa Tume ya Ulaya amepinga kauli hiyo akisema kuwa ikiwa haki za msingi kama vile za kijamii kiutu na za kibinadamu zimewekwa imara maslahi ya taifa yatashughulikiwa vizuri.
“ Mawili hayo huenda sambamba.Ni kile ninachoiweza kuita usalama endelevu. Hakuna usalama endelevu bila kujumulisha haki kwa wote. Tuko hapa kuonyesha kuwa kila maslahi ya taifa lolote ni kulinda haki za binadamu za raia wake wote. Kila ukiukwaji wa haki za binadamu ni kwenda kinyume na juhudi zetu sote na kwa ajili ya maslahi ya mataifa yetu. Yote yanakwenda sambamba.”
Naye Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Bi Michelle Bachelet, akitoa kauli yake wakati wa uzinduzi huo uliohudhuriwa na wadau mbalimbali wa haki za binadamu kutoka nchi 14 na Umoja wa Ulaya, amesema kuwa ushirika mpya wa kutoa habari nzuri kuhusu haki za binadamu utaleta manufaa, akitoa mfano wa habari njema kuhusu mkataba wa amani kati ya Ethiopia na Eritrea.
“ Baada ya miaka 20 ya uhasama nimefurahia jinsi watu wa mataifa hayo walivyopokea kwa furaha makubaliano hayo na ni kwa sababu nzuri.Matokeo ya haraka ni kurejelea mawasiliano ya simu , safari za ndege , na viongozi wa mataifa hayo mawili kuahidi kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kisasia wa nchi hizo na kuona kama maendeleo ya amani na ushirikiano zaidi vinatanda katika eneo zima la pembe ya Afrika.”
Pia ametoa mfano mwingine kuhusu kile kilichotokea Afrika Kusini na Chile ambako ubaguzi wa rangi uliondolewa na kufanyika uchaguzi wa wote na kuheshimu haki za binadamu katika nchi hizo na hivyo amani kupatikana na hivyo haki za binadamu kuheshimika.
Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , Antonio Guterres naye alizungumza na kusema kuwa kuheshimu na kuendeleza haki za binadamu ni msingi wa upanuaji wa upeo wa matumaini na kuvuka mipaka ili keleza mazuri kwa maslahi ya jamii bora, akiongeza kuwa kawaida kile kinachovutia ulimwengu huu ni habari mbaya kama vile changamoto za haki za binadamu na mabaya yake.
Ameongeza kuwa haki za binadamu ni chombo cha kumuendeleza mwanadamu.
Tukio hili pia linatumiwa kama sherehe ya kuadhimisha miaka 70 ya tamko la haki za binadamu na pia miaka 25 ya kutangazwa kwa mpango tekelezi wa Vienna na vilevile miaka 20 ya tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wanaotetea haki binadamu duniani.