Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake walikuwa na mchango mkubwa katika kuandikwa kwa tamko la haki za binadamu

Mtafiti Rebecca Adami akiwa katika studio za UN News kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani.
UN News/Paulina Greer
Mtafiti Rebecca Adami akiwa katika studio za UN News kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani.

Wanawake walikuwa na mchango mkubwa katika kuandikwa kwa tamko la haki za binadamu

Wanawake

Wiki ijayo, dunia itaadhimisha miaka 70 ya tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu. Ingawa historia ya dunia inaonekana kuwasahau wanawake, mtafiti wa masuala ya haki za binadamu Dkt Rebecca Adami katika kitabu chake cha ‘Wanawake na tamko la haki za binadamu’ anasema wanawake walikuwa na mchango mkubwa katika kuliandaa na kulitekeleza tamko hilo.

Rebecca anasema wanawake kutoka nje ya Ulaya na marekani, licha ya kuwa na mchango mkubwa katika kuundwa kwa tamko hilo mchango wao haujapewa uzito unaositahili katika historia.

Mathalani akiwazungumzia wajumbe waliokuwa na ushawishi mkubwa katika maazimio hayo, kama Bi. Minerva Bernardino wa Jamhuri ya Dominica, Bi. Hansa Mehta kutoka India na Bi. Begum Shaista Ikramullah wa Pakistan.

Kuhusu mchango wa wanawake kutoka Afrika katika tamko hilo Bi. Rebecca akizungumza na UN News amesema ni mwanamke mmoja tu aliyetajwa kutoka Liberia.

“Alikuwa ametajwa katika moja ya kumbukumbu za mikutano ya Baraza Kuu la Umoja wa mataifa, na nilipoona hilo nikashawishika kuwa hiyo itakuwa kazi yangu inayofuata, nahitaji kufuatilia mchango wa wanawake wa Afrika”

Rebecca anasema wanawake wa Afrika walikuwa na mchango mkubwa ambao haujaangaziwa na hilo linamsukuma zaidi kulifanyia kazi.

"Kwa sababu katika miaka ya 1950 na 1960 baada ya kuidhinishwa kwa tamko la haki za binadamu, wanawake hao walikuwa na mchango muhimu wakati nchi zao zikiwa chini ya usimamizi wa mataifa mengine na hata katika kupigania uhuru dhidi ya ukoloni kwa hivyo nafikiri hili ni jambo ambalo linasitahili kuangaziwa, katika historia ya Umoja wa Mataifa”

 Wanawake kutoka Japan wakitizama tamko la haki za binadamu walipotembelea makao makuu ya muda ya Umoja wa Mataifa Feb 1950 yaliyokuwa Lake Success, New York Marekani.
UN Photo.
Wanawake kutoka Japan wakitizama tamko la haki za binadamu walipotembelea makao makuu ya muda ya Umoja wa Mataifa Feb 1950 yaliyokuwa Lake Success, New York Marekani.

Tamko la haki za binadamu liliidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 10 Desemba mwaka 1948 baada ya kushuhudiwa ukatili uliotokana na vita kuu ya pili ya dunia pamoja na msururu wa matendo ya ukiukwaji wa haki za binadamu ulimwenguni kote.