Mfuko wa manusura wa utesaji ni mkombozi kwa manusura na familia zao

7 Novemba 2018

Ibara ya 5 ya tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa linalotimiza miaka 70 mwaka huu wa 2018, inaweka bayana kuwa hakuna mtu yeyote anayepaswa kuteswa kwa sababu yoyote ile. 
 

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimetia saini na kuridhia tamko hilo lakini bado baadhi zinatuhumiwa kutesa watu kwa sababu mbalimbali jambo linaloleta ulemavu, madhara ya kisaikolojia na hata wengine hujiua. 

Ni kwa kuzingatia uwepo wa vitendo kama hivyo, mwaka 1981, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilianzisha mfuko wa hiari kwa manusura wa utesaji ukilenga kusaidia manusura wenyewe na familia zao.

Wavuti wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, inasema kuwa mfuko unasaidia manusura na familia zao kujenga upya maisha yao na kupatia suluhu vitendo vya ukiukwaji haki ambavyo wamepitia.

MFUKO UNASAIDIA NANI?
 

Mfuko huu unasaidia manusura wa mateso popote pale walipo mwaka 2015, ulitoa msaada wa moja kwa moja kwa manusura 57,000, wakiwemo watu wazima na watoto waliopo kwenye nchi zaidi ya 80.
Makundi hayo ni pamoja na wasaka hifadhi, wahamaji wasio na nyaraka, manusura wa ukatili wa kingono kwenye vita, watetezi wa haki za binadamu watu walitoweshwa , watu wa jamii ya asili,  watu waliobadili jinsia.

AINA ZA MIRADI AMBAYO HUPATIWA FEDHA
 

Miradi ni pamoja na vituo vya kuraghbisha manusura, mashirika ya kiraia, vikundi vya manusura na waliotoweshwa, hospitali za umma na binafsi, vituo vya msaada wa kisheria.

JE MANUSURA WA MATESO WANASEMAJE?
 

Je ni kwa kiasi gani madhila hayo yanakumba watu? Na huwa wanajisikia vipi wakati wa mateso na hata baada ya mateso? Jamii zao je? Basi  ungana na Assumpta  Massoi kwenye makala hii iliyowezeshwa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR.
 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter