Skip to main content

Mtoto mmoja kati ya watatu CAR anahitaji msaada wa kibinadamu- Ripoti UNICEF

UNICEF imesema Novemba 2018 kuwa watoto wawili kati ya watatu wanahitaji msaada wa kibindamu.
UNICEF/Ashley Gilbertson
UNICEF imesema Novemba 2018 kuwa watoto wawili kati ya watatu wanahitaji msaada wa kibindamu.

Mtoto mmoja kati ya watatu CAR anahitaji msaada wa kibinadamu- Ripoti UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF imesema watoto milioni 1.5 nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wanahitaji msaada wa kibinadamu ikiwa ni ongezeko la watoto laki tatu tangu 2016.

Ripoti hiyo iliyopatiwa jina, “Janga CAR: Katika mzozo uliosahaulika, watoto wanahitaji msaada, ulinzi na mustakabali" inaonesha kuwa takriban watoto 43, 000 walio chini ya umri wa miaka mitano wanakadiriwa kuwa kwenye hatari ya kufariki dunia kutokana na utapiamlo uliokithiri. 

Ripoti inaongeza kuwa maelfu ya watoto wako katika vikundi vilivyojihami kwa silaha na maelfu wako hatarini kukumbwa na ukatili wa kingono.

Akizungumzia hali CAR mwakilishi wa UNICEF nchini  humo Christine Muhigana, amesema..

(SAUTI YA CHRISTINE MUHIGANA)

“Mzozo wa CAR huenda ni mzozo uliosahaulika zaidi duniani. Unafanyika katika taifa maskini kabisa na wahudumu wa kibinadamu wako katika maeneo hatari. Hali ya watoto ni ya kusikitisha na mtoto mmoja kati ya wanne amefurushwa au ni mkimbizi. Lakini kwa kweli watoto wote katika nchi hii wanahitaji aina moja ya msaada, watoto wa CAR wametelekezwa kwa muda mrefu. Wanahitaji kuangaliwa. Wanahitaji msaada sasa. Wanahitaji kwa siku za baadaye ili wawe na mustakabali ambao unawapa matumaini na ambao wangeupenda.”

UNICEF inajizatiti kusaidi watoto walio na mahitaji ya dharura ikiwemo: kusambaza chakula kwa walio na utapiamlo uliokithiri, kutoa chanjo kwa watoto dhidi ya magonjwa hatari, kuweka sehemu za muda za kutoa elimu na mafunzo kwa watoto, kusaidi watotowalioachiliwa kutoka kwa makundi yaliyojihami na kufikisha kwa haraka na mahitaji ya kuokoa maisha kwa jamii zilizoko hatarini.

Licha ya mahitaji mengi yanayochangiwa na kuongezeka kwa machafuko ni asilimia 44 tu ya ombi la dola milioni 56.5 la UNICEF kwa 2018 ndio imefadhiliwa kufikia mwisho wa mwezi Oktoba.