Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano Birao nchini CAR yamesababisha janga kwa wakazi-OCHA

Wanawake na watoto wakimbizi wa ndani kwenye mji wa Paoua nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.
Yaye Nabo Sène/OCHA
Wanawake na watoto wakimbizi wa ndani kwenye mji wa Paoua nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Mapigano Birao nchini CAR yamesababisha janga kwa wakazi-OCHA

Amani na Usalama

Mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Denise Brown amesema mapigano katika mji wa kasakzini Mashariki mwa nchi hiyo wa Birao, jimbo la Vakaga ,yamesababisha janga kwa wakazi na ni ukiukaji wa haki za binadamu.

Kupitia taarifa ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA iliyotolewa Bangui leo Jumanne Bi. Brown amesema, “mapigano mjini Birao katika kipindi cha wiki mbili yamesababisha familia kukimbia makwao na kusaka hifadhi mbali na maneoe kunakoshuhudia mapigano; nyumba zimetekezwa na kumekuwa na uporaji.”

Kufuatia mapigano ya Septemba Mosi na Septemba 14, takriban watu 13,000 hususan wanawake na watoto wamelazimika kukimbia makazi yao nakusaka hifadhi.

Licha ya ukosefu wa usalama na changamoto za kufikia maeneo katika muda wa saa 48 ya mapigano mnamo Septemba mosi, wadau wa kibinadamu walipeleka wafanyakazi zaidi na vifaa vya makazi ya muda, dawa, lishe na chakula.

Bi. Brown ameongeza kwamba, “usambazaji ni lazima uendelee ili kuhakikisha kwamba mahitaji ya waliofurushwa yanafikiwa katikati ya mzozo. Ukatili ni lazima ukomeshwe kuhakikisha uwasilishaji wa msaada.

Mratibu huyo wa misaada ametoa wito kwa pande zote kuzingatia wajibu wao chini ya sharia ya kimataifa na kulinda raia, miundombinu na wahudumu wa kibinadamu.

Aidha ametoa wito kwa wafadhili kuimairisha msaada wa kibinadamu kwa ajili ya CAR kwani idadi ya watu walio na mahitaji ya dharura inatarajiwa kuongezeka.

Ombi la msaada kwa ajili ya CAR limefadhiliwa kwa nusu tu wakipokea dola milioni 207.9 ikilinganishwa na dola milioni 430.7 lililotolewa.