Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wengine wanaweza kusema huwezi kupambana na mabadiliko ya tabianchi na ukawa na uchumi mzuri. Ninakataa!-Guterres

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akijibu maswali ya wanahabari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York 28 November 2018.
UN Photo/Rick Bajornas)
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akijibu maswali ya wanahabari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York 28 November 2018.

Wengine wanaweza kusema huwezi kupambana na mabadiliko ya tabianchi na ukawa na uchumi mzuri. Ninakataa!-Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo akiwa mjini New York Marekani kabla ya kusafiri kwenda Argentina unakofanyika mkutano wa nchi 20 zilizoendelea zaidi kiuchumi G20,  amewaambia wanahabari kuwa changamoto kubwa hivi sasa ni ukosefu wa kuaminiana duniani.

 

Amesema, “dunia yetu inakabiliana na mgogoro wa kukosa imani. Wale ambao wameachwa nyuma na utandawazi wanakosa kuziamini serikali na taasisi. Kukosekana kwa usawa kumeenea na kuongezeka hususani ndani ya mataifa.”

Zaidi ya hayo amesema  migogoro ya biashara inaongezeka na hali ya mvutano wa kijiografia inaongeza shinikizo zaidi kwa uchumi wa dunia. Ni muhimu tushughulikie sababu za msingi na kufanya kazi pamoja ili kukuza utandawazi ulio wa haki”

Guterres amesisitiza kuwa malengo ya maendeleo endelevu SDGs ni chachu muhimu kwa utandawazi ulio wa haki na ana matumaini kuwa viongozi wa G20 watakubaliana naye.

Amesema, “wengine wanaweza kusema huwezi kupambana na mabadiliko ya tabianchi na ukawa na uchumi mzuri. Ninakataa kwa nguvu zote. Kimsingi kinyume chake ndicho sahihi. Gharama za kijamii, kiuchumi na kimazingira zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi ni ndogo kulinganisha na kuchukua hatua sasa.”

Amesisitiza kuwa kushindwa kuchukua hatua kunamaanisha majanga zaidi na dharura na uchafuzi wa hewa ambavyo  amesema vinaweza kuugharimu uchumi wa dunia kufikia dola za kimarekani trilioni 21 kufikia mwaka 2050.

Picha ya sayari ya dunia kutumia sateliti. Mabadiliko ya tabianchi yanaiweka hatarini dunia na viumbe vilivyomo.
NASA
Picha ya sayari ya dunia kutumia sateliti. Mabadiliko ya tabianchi yanaiweka hatarini dunia na viumbe vilivyomo.

 

Guterres ameongeza kusema kuwa kushughulikia mabadiliko ya tabianchi ni fursa na teknolojia iko upande wetu. Na biasahara ya kijani ni biashara nzuri.

Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, “wanachama wa G20 wanawajibika zaidi ya robo tatu ya uchafuzi wa hali ya hewa na pia wakati huo huo wanachama wa G20 wana nguvu ya kuibadili hali hiyo. Pia wana rasilimali za kutoa misaada ya kifedha inaayotakiwa kuirejeshaa hali kaatika ubora wake.”

Guterres ambaye baada ya mkutano wa G20 huko Argentina ataelekea Poland katika mkutano 24 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP24, , amesema anaenda na ujumbe huo huo katika mikutano yote miwili kuwa kuzuia hewa chafu ya ukaa ni jambo linalowezekana lakini “tunahitaji nia kubwa na tuko katika mbio kwa ajili ya mstakabali wa maisha yetu yajayo na kwamba ni mbio ambazo tunaziwezaa na tunatakiwa kushinda.”

Kulingana na takwimu za shirika la afya duniani WHO, zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa mijini kote duniani wanavuta hewa chafu.

Nalo shirika la hali ya hewa duniani WMO limegundua hewa chafu ya ukaa katika anga imeongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miaka milioni 3.