Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maafisa wa mipaka ya Tanzania na Burundi wanolewa na IOM ili kusimamia vizuri mipaka

Wakimbizi kutoka Burundi wakichota maji ukimbizini
UNHCR/Colin Delfosse
Wakimbizi kutoka Burundi wakichota maji ukimbizini

Maafisa wa mipaka ya Tanzania na Burundi wanolewa na IOM ili kusimamia vizuri mipaka

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM linashirikiana na serikali za Tanzania na Burundi katika kujengea uwezo taasisi zao za mipakani ili ziweze kushughulikia kwa ufanisi uvukaji wa watu  wengi mpakani kupitia mfumo wa udhibiti wa mipaka kibinadamu, HBM.

Taarifa ya IOM iliyotolewa leo  huko Bujumbura, mji mkuu wa Burundi  na Dar es Salaam mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania imemnukuu mkuu wa shirika hilo ofisi ya Tanzania,Qasim Sufi akisema kuwa, “kuimarisha stadi na uelewa wa maafisa wa mpakani kutoka Burundi na Tanzania kwa mujibu wa mfumo wa HBM ni jambo la umuhimu kwani mpaka kati nchi mbili hizo unashuhudia uvukaji mkubwa wa watu kutokana na migogoro ya kibinadamu.”

Mradi wa kuwanoa maafisa wa mpakani mwa Burundi na Tanzania, ni wa miezi 12 na unatekelezwa  kwa pamoja na mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa, IOM, lile la mpango wa maendeleo, UNDP na lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na lengo lake ni kuleta amani mpakani wa Burundi na Tanzania kupitia mwelekeo madhubuti wa mpakani, ambao unaegemea  haki za binadamu, na kuhusisha mashirika kadhaa ambao unaungwa mkono na fuko la ujenzi wa amani la Umoja wa Mataifa.

Wajibu wa IOM katika mradi huu ni kuratibu uchanganuzi, kujenga uwezo baina ya washika dau na pia kuweka  utaratibu wa kufuatwa katika operesheni SOP, pamoja na kuitisha na kusimamia mikutano na warsha kuhusu mipaka kati ya maofisa wa mpakani wa  nchi hizo mbili.

Hadi sasa maafisa wa uhamiaji pamoja na askari polisi wa mpakani 64 kutoka Burundi na Tanzania, wamepewa mafunzo kuhusu HBM ambapo baadhi ya mafunzo yalifanyika Bujumbura, Burundi ilhali mengine Kigoma Tanzania.

Awali IOM ilifanya  tathmini mbili katika  kituo cha Muguna mkoa wa Makamba na pia Gisuru ,mkoa wa Ruyigi nchini Burundi na upande wa Tanzania ilikuwa  Manyovu, wilaya ya Buhigwe na pia Mabamba  wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.

 IOM inasema tathmini yao ilidhihirisha kuwepo kwa hali ya kutojitayarisha vema kuhusu hali ya dharura upande wote wa mpaka huo ambao una uvukaji wa kiholela hususan wakati wa migogoro upande wa Burundi au wakati wa zoezi la kuwarejesha kwa hiari  nyumbani wakimbizi kutoka Tanzania.

Mbali na uvukaji unaosababishwa na migogoro pia IOM imegundua kuwa mipaka hiyo iko katika sehemu yenye magonjwa kadhaa kama vile kipindupindu na Ebola.