Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Burundi wapata ajali Ngara

Kambi ya wakimbizi wa Burundi ya Nduta iliyoko nchini Tanzania.(Picha:UNHCR/Sebastian Rich)

Wakimbizi wa Burundi wapata ajali Ngara

Amani na Usalama

Idadi kubwa ya wakimbizi wa Burundi wanahofiwa kufariki dunia baada ya mabasi walimokuwa wakisafiria kurejea nyumbani kutoka Tanzania kupata ajali mkoani Kagera, kaskazini-magharibi mwa Tanzania.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema wakimbizi 515 wa Burundi walikuwa wakisafiri katika jumla ya mabasi 8 kutoka kambi ya Nduta kuelekea kituo cha mpito cha mapokezo kilichopo jimbo la Ngozi nchini Burundi.

UNHCR imesema ni wakati wa msafara huo ndipo mabasi mawili yaliyokuwa mbele yaligongana na kupinduka ambapo hali mbaya ya hewa imetajwa kuwa sababu ya ajali hiyo. Kila basi lilikuwa na abiria 64.

 

Image
Wakimbizi wa Burundi. (Picha:UNHCR/Federico Scoppa)

Hivi sasa UNHCR inashirikiana na serikali ya Tanzania, mamlaka za serikali za mitaa na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la uhamiaji, IOM na la mpango wa chakula, WFP pamoja na mashirika ya kiraia kusafirisha majeruhi hadi hospitali ya wilaya ya Nyamiaga.

Halikadhalika wanashirikiana ili kupata rasilimali zinazohitajika kusaidia majeruhi ikiwemo dawa na chakula.

UNHCR imeeleza masikitiko  yake kufuatia tukio hilo ambalo limehusisha pia wafanyakazi wawili wa IOM waliokuwa wanasindikiza wakimbizi hao hadi mpakani mwa Tanzania na Burundi.

Na kupitia taarifa yake, shirika hilo limetuma salamu za rambirambi kwa waathirika na familia zao.