Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Warohingya huko Kutupalong wapatiwa mitungi ya gesi ili kulinda afya na mazingira

Warohingya katika kambi ya Kutupalong wakisaidia ujenzi kwenye kambi yao huko Bangladesh
WFP/Saikat Mojumder
Warohingya katika kambi ya Kutupalong wakisaidia ujenzi kwenye kambi yao huko Bangladesh

Warohingya huko Kutupalong wapatiwa mitungi ya gesi ili kulinda afya na mazingira

Wahamiaji na Wakimbizi

Huko Cox’s Bazar nchini Bangladesh ambako kuna kambi   ya Kutupalong inayohifadhi wakimbizi wa kabila la Rohingya kutoka Myanmar, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,  UNHCR limeanza kusambaza mitungi ya gesi kwa lengo la kuwezesha wakimbizi hao kutumia nishati salama na endelevu.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi, Andrej Mahecic ameaambia waandishi wa habari kuwa mradi huo ni sehemu ya usaidizi wa kibinadamu na unalenga kufikia kaya 200,000 za wakimbizi pamoja na baadhi ya familia za wenyeji zinazowahifadhi.

“Mitungi hiyo  ya gesi itakuwa ni chanzo bora cha nishati kwa ajili ya kupikia na hata kuweka joto ndani ya nyumba na hivyo pamoja na kusaidia kuondoa adha ya moshi itabadili pia mwelekeo wa uharibifu wa mazingira unaotokana na uwepo wa wakimbizi hao kwenye eneo hilo la kusini mwa Bangladesh,” amesema Bwana Mahecic.

UNHCR inasema hadi sasa, wakimbizi hao warohingya na jamii nyingi zinazowahifadhi wamekuwa wakitumia zaidi kuni kama chanzo cha nishati na kwamba “familia za wakimbizi zinatumia muda mrefu kuchanja kuni au hutumia fedha kidogo walizo nazo kununua kuni.”

Mradi wa majaribio uliofanyika msimu huu wa pukutizi kujaribu kusambaza mitungi hiyo ya gesi kwa kaya 6,000  umeonyesha kuwa kitendo hicho kinapunguza ukataji miti hovyo na pia kinaepusha wakimbizi wanaosaka kuni, hususan wanawake na wasichana dhidi ya vitendo hatarishi.

“Matumizi ya gesi pia yataboresha kiwango cha hewa na afya ya watumiaji kwa kuwa wakimbizi hawatatumia tena kuni au nishati nyingi hatarishi kupikia,” amesema Mahecic akiongeza kuwa wahudumu wa afya huko Kutupalong walibaini kuwa magonjwa ya njia ya hewa miongoni mwa wakimbizi yanachochewa na moshi.

Mradi huo wa kusambaza nishati mbadala ya gesi kwa wakimbizi unafadhiliwa kwa pamoja na serikali ya Bangladesh na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la chakula na kilimo, FAO, uhamiaji, IOM na mpango wa chakula, WFP.


Mgao huo unaenda sambamba na kuelimisha wakimbizi matumizi salama ya mitungi hiyo ya gesi.