Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani watatu wa MINUSCA kutoka Tanzania wamejeruhiwa nchini CAR 

Mlinda amani wa MINUSCA akiwa katika doria nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR-Kutoka Maktaba
MINUSCA/Herve Cyriauqe Serefi
Mlinda amani wa MINUSCA akiwa katika doria nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR-Kutoka Maktaba

Walinda amani watatu wa MINUSCA kutoka Tanzania wamejeruhiwa nchini CAR 

Amani na Usalama

Walinda amani watatu wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzaina wanaohudumu katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ujulikanao kama  MINUSCA wamejeruhiwa jana Alhamisi katika kijiji cha Batouri Bole, mkoani Mambéré-Kadéï baada ya gari lao kukanyaga kilipuzi. 

Taarifa ya MINUSCA inasema mlinda amani mmoja hali yake ni mbaya na wote wamesafirishwa kwenda mji mkuu Bangui kwa matibabu zaidi. 

Mlinda amani  aliyejeruhiwa vibaya alisafirishwa hadi Bouar kwa matibabu huko kabla ya kuhamishwa mjini Bangui.

Tukio hilo lilitokea mwendo wa saa tano asubuhi  saa za Jamhuri ya Afrika ya Kati wakati msafara wao ulipokuwa ukiondoka katika mji wa Berbérati kuelekea vituo vya muda vya jeshi kwenye maeneo ya Gbambia na Amada-Gaza, miji iliyo karibu kilomita 100 kaskazini mashariki mwa Berbérati.

MINUSCA inalaani vikali utumiaji wa vilipuzi unavyofanywa na vikundi vilivyojihami katika maeneo mbalimbali nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambavyo tayari vimesababisha makumi ya vifo na majeruhi miongoni mwa rai ana walinda amani.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini CAR na  na mkuu wa MINUSCA anawatakia ahueni ya haraka walinda amani waliojeruhiwa .

"Licha ya hali ngumu ya walinda amani wetu ardhini, ikichochewa na kuwepo kwa vilipuzi vilivyoboreshwa, MINUSCA bado imeazimia kwa dhati kutekeleza majukumu yake yakuleta amani na utulivu nchini CAR," amesema mwakilishi huyo Mankeur Ndiaye.

Hii ni mara ya tatu kwa walinda amani wa MINUSCA kujeruhiwa na vilipuzi nchini CAR.