Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vaa nguo ya buluu tarehe 20 Novemba kuunga mkono kampeni ya watoto

Wasichana wakiwa ndani ya hema kaskazini mwa Syria.2018
UNICEF/ Aaref Watad
Wasichana wakiwa ndani ya hema kaskazini mwa Syria.2018

Vaa nguo ya buluu tarehe 20 Novemba kuunga mkono kampeni ya watoto

Masuala ya UM

Kuelekea siku ya watoto duniani tarehe 20 mwezi huu wa Novemba, mtoto muigizaji Millie Bobby Brown ameungana na mabalozi wema wa shirika la kuhudumia watoto duniani,  UNICEF kutumia video mahsusi kupigia chepuo kampeni ya kusongesha haki za watoto duniani. 

Sauti  kutoka katika video iliyomshirikisha mtoto Millie mwenye umri wa miaka 14 pamoja na waigizaji nguli Orlando Boom, Liam Neeson na Lilly Singh pamoja na mwimbaji na mtunzi Dua Pipa.

Rangi iliyotamalaki ni ya buluu ikibeba maudhui ya kampeni hii ya kuvaa au kuonyesha rangi ya buluu kwa mazingira yoyote kama ishara ya kuandaa mazingira ya ustawi kwa watoto.

Millie kajipatia jina la Blue na akiwa amevalia nguo ya buluu, yuko kwenye mandhari ya ofisi anapiga simu akitoa amri kwa makundi mbalimbali ya watoto na watu wazima wavae au wahakikishe wana rangi ya buluu.

Hata wapiga rangi nao na makopo yao wanaamrishwa wahakikishe wana rangi ya bluu!

Kisha…Dawati la ufundi! Wataalamu wa mavazi..

Sasa lazima tuwashirikishe marafiki, anampigia simu Liam….Orlando…Lily na Du. Kisha Millie anasema,“Katika siku ya watoto duniani, UNICEF inatoa wito kwa watoto na watu wazima kote duniani, kuwa na rangi  ya buluu ili kuunga mkono haki za watoto. Kwa kuwa na rangi ya buluu na kutia saini ombi letu, unaeleza dunia kuwa unaamini katika ulimwengu wenye ustawi wa watoto na kusaidia UNICEF ifanikishe ndoto hiyo.”

Ombi hilo la kutia saini linapatikana katika  wavuti wa Uniceg ambapo mtu yeyote mwenye umri wa zaidi ya miaka 13 anaweza kujaza na kuwasilisha kuonyesha azma yake ya kuona haki za mtoto zinazingatiwa.

Haki hizo kwa mujibu wa mkataba wa haki za mtoto duniani, CRC ni kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa ambapo ombi hilo lenye saini litawasilishwa kwa wakuu wa nchi na serikali mwakani.