BTS yatoa video maalum, “saka upendo ndani yako uweze kusambaza kwa wengine”

30 Julai 2019

Wanamuziki vijana wa kikundi mashuhuri cha muziki duniani, BTS ambao pia ni waungaji mkono wa kazi za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF wametoa wito kwa vijana kueneza wema katika siku hii ya leo ya kimataifa ya urafiki.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo mjini Seoul, Korea Kusini na New York, Marekani imesema vijana hao wametoa wito huo kupitia video ya kipekee waliyoitoa leo wakitaka vijana kutumia wema ili kuchangamsha siku ya mtu ikiwa ni sambamba na kampeni ya shirika hilo ya kutokomeza ghasia ndani na nje ya shule.

UNICEF inasema duniani kote, wanafunzi milioni 150, nusu yao wakiwa na umri wa kati ya miaka 13 hadi 15 wameelezea kukumbwa na vitendo vya kikatili kutoka kwa wenzao wa rika lao iwe shuleni au nje ya shule.

Ni kwa mantiki hiyo kundi hilo la BTS la Korea Kusini kupitia video hiyo imeimba wimbo uitwao Answer- Love myself au Jibu – Jipende mwenyewe, ukiwa na mashairi ya simulizi za kutunga za watoto na vijana wanaokumbwa na ukatili, manyanyaso na hofu wanapokuwe nje na ndani ya shule.

“Kadri simulizi hiyo inavyoendelea, watazamaji wanaona mabadiliko ya tabia pindi vijana wa rika moja wanapoanza kuonesha urafiki, kusaidia na kuwapenda wale ambao wanakumbwa na manyanyaso au wanaoumizwa,” imesema taarifa hiyo ya UNICEF.

 “Kampeni yetu ya jipende mwenyewe ni kuhusu kuwahamasisha vijana kusaka upendo kuanzia ndani  yao wenyewe na kisha wausambaze kwa wengine,” wamesema wanamuziki hao wa BTS wakiongeza kuwa “tunataka kila mtu awe sehemu ya kutokomeza ukatili kwa kusambaza upendo na wema.”

Video hii ni sehemu ya kampeni ya BTS ya #JipendeMwenyewe, au LOVE MYSELF, ambayo imeshachangisha zaidi ya dola milioni 2 kusaidia kufanikisha kampeni ya UNICEF ya kutokomeza ghasia au #ENDviolence ndani na nje ya shule.

Mwezi Desemba mwaka jana, watoto na vijana kutoka maeneo mbalimbali duniani walichapisha ilani  ya vijana ya kutokomeza ukatili, au #ENDviolence Youth Manifesto ikitoa wito kwa serikali, walimu, wazazi na kila mtu kusaidia kutokomeza ukatili na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanajisikia salama wanapokuwa shuleni wanapokuwepo nje na ndani ya shule kwa kuazimia kuwa wema na wenye heshima.

Kwa sasa UNICEF inakaribisha watoto na vijana kuchukua hatua ya kwanza kwa kuwa wema kwa mtu kupitia andiko la kwenye mtandao au kumpatia mtu andiko hilo moja kwa moja.

 “Watoto na vijana wametueleza kila mara ya kwamba kutendewa wema na kwa huruma na kwa heshima kunawasaidia kujisikia salama ndani na nje ya shule,” amesema Henrietta Fore, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter