Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rangi ya buluu ikitawala, Beckham asema "siku zijazo ni za watoto wetu hivyo tutunze ndoto zao"

Rangi ya buluu iliangaza ndani ya ukumbi wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC.
UN Photo/Manuel Elías
Rangi ya buluu iliangaza ndani ya ukumbi wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC.

Rangi ya buluu ikitawala, Beckham asema "siku zijazo ni za watoto wetu hivyo tutunze ndoto zao"

Haki za binadamu

Mustakabali si wa kwetu bali ni wa watoto wetu kwa hiyo tuchukue hatua zaidi kulinda ndoto za watoto, amesema David Beckham, Balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, wakati akihutubia hii leo kikao cha ngazi  ya  juu cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kilichofanyika kuadhimisha miaka 30 tangu kupitishwa kwa mkataba wa haki za mtoto, CRC na sambamba na siku ya mtoto duniani,

 

Beckham amesema “sisi kama viongozi, watu mashuhuri, wazazi na pia binadamu tuchukue hatua zaidi,”  huku akirejelea  uzoefu wake wakati akitembelea watoto maeneo mbalimbali duniani akisema kuwa, watoto wanataka kuwepo kwa dunia ambayo itasaidia siyo tu wao bali pia vizazi vijavyo, ambako rasilimali zitakuwa endelevu na mazingira yatalindwa.”

Amesema watoto pia wanataka amani na kutokomezwa kwa vita na migawanyiko ya kisiasa na kitamaduni ambayo husambaratisha jamii zao, familia na kuhatarisha maisha ya watoto kila uchao.

Millie Bobby Brown ambaye pia ni Balozi mwema wa UNICEF ameangazia zaidi suala la uonevu akisema kuwa, “nashawishika kuwa mitandao ya kijamii haipaswi kuwa pahala pa hofu, uonevu na manyanyaso. Inaweza kuleta watu pamoja na inaweza kuwa pahala pa upendo na kusaidiana.”

Ameongeza kuwa, “pahala fulani hivi sasa duniani, msichana anaonewa mtandaoni. Ana hofu, yuko hatarini na anajiona mpweke. Ujumbe wangu kwake ni kwamba, Hauko peke yao, kuna watu ambao wanakujali na kuna watu watakusikiliza iwapo utapaza sauti kuomba msaada.”

Balozi mwema wa UNICEF, David Beckham akizungumza wakati wa kikao cha ngazi ya juu cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika kuadhimisha miaka 30 tangu kupitishwa kwa mkataba wa haki za mtoto duniani, CRC. (20 Novemba 2019)
UN Photo/Manuel Elías
Balozi mwema wa UNICEF, David Beckham akizungumza wakati wa kikao cha ngazi ya juu cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika kuadhimisha miaka 30 tangu kupitishwa kwa mkataba wa haki za mtoto duniani, CRC. (20 Novemba 2019)

Akipazia sauti hoja ya msichana wa rika lake ambaye ni mwanaharakati wa mazingira Greta Thunberg, Millie amesema kwamba vijana kama Greta wanapaza sauti ili viongozi wa dunia wasikilize na wachukue hatua.

Amehamasisha watoto walioshiriki tukio hilo na kuwaambia kuwa, “kila mmoja wenu aliyepo hapa anaweza kuwa kipaza sauti kinachoweza kubadili sauti zetu na kuleta mabadiliko ya kweli kuwa sera, sheria na uwekezaji ambao unaweka watoto salama, dunia iwe bora, salama na thabiti kwa ajili ya wote.”

Henrietta Fore, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF akihutubia washiriki wa tukio hilo amesema kuwa, “njia bora zaidi ya kuwa na mustakbali endelevu kwa wote ni kuwekeza kwa watoto.”

Bi. Fore ameseam kuwa leo hii wakati ulimwenguni unamulika miaka 30 ijayo ya CRC, “hebu na tuweke tena ahadi ya kuzingatia haki za mtoto, hebu na tufanye haki hizi ziwe za uhalisia kwenye mipango yetu, sera na huduma katika kila jamii na katika kila nchi duniani kote.”

Jengo la Baraza la Wawakilishi Ethiopia liliangazia rangi ya buluu kuashiria kuunga mkono haki za mtoto.
© UNICEF/UN0346330/Sewunet
Jengo la Baraza la Wawakilishi Ethiopia liliangazia rangi ya buluu kuashiria kuunga mkono haki za mtoto.

Majengo muhimu duniani yaangaza rangi ya buluu

Katika kuadhimisha siku ya mtoto duniani majengo muhimu duniani kote yaliangazia rangi ya buluu ikiwa ni alama ya umoja.

Huko Christchurch, New Zealand, msikiti wa Al Noor , eneo ambako kulifanyika shambulizi dhidi ya waislamu mwezi Machi mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 51, rangi ya buluu ilimulika kuonesha mshikamano.

Nchini Ugiriki, jengo l aAcropolis mjini Athens liling’ara na rangi ya buluu, na hii ikiwa mara ya kwanza kwa eneo hilo la urithi wa dunia linalotambuliwa na UNESCO kuonekana na rangia.

Barani Afrika  hususan nchini Ethiopia, katika mkesha wa miaka 30 ya CRC, jengo la Baraza la Wawakilishi liliangazia rangi ya buluu kuashiria kuunga mkono haki za mtoto. Bi. Abeba  Yosef, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati  ya Baraza hilo kuhusu masuala ya kijamii pamoja na Adele Kohdr, Mwakilishi wa UNICEF nchini Ethiopia waliwasha kitufe cha kuangazia jengo hilo rangi ya buluu.

Baadaye leo hapa jijini New York, Marekani, Balozi wa UNICEF nchini China, Wang Yuan atawasha rangi ya buluu kwenye jengo la Empire State ambalo ni moja ya alama za New York, na leo itakuwa ni mara ya pili mfululizo kwa jengo hilo kuangaza rangi ya buluu wakati wa siku ya mtoto duniani.