UN yaondoa vikwazo dhidi ya Eritrea

14 Novemba 2018

Baraza la  Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio la kuondoa vikwazo dhidi ya Eritrea ambavyo nchi hiyo ilikuwa imewekewa tangu mwaka 2009, hatua hiyo ikielezwa kuwa ya kihistoria. 

Akiwasilisha azimio hilo mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama, mwakilishi wa kudumu wa Ethiopia kwenye Umoja wa Mataifa balozi Taye Atske Selassie amesema hatua ya leo inazingatia maendeleo ya kisiasa kwenye pembe ya Afrika, ikiwemo maelewano ambayo yamegeuza mzozo kuwa fursa za ushirikiano na usalama.

Kwa mantiki hiyo azimio hilo linaondoa maazimio manne; la mwaka 2009, 2011, 2012 na 2013 ambayo yaliweka vikwazo vya silaha, safari na kuzuia mali, yakilenga Eritrea pamoja na Somalia, ambapo sasa azimio linasema kuwa kamati iliyoanzishwa na maazimio hayo ikilenga nchi mbili hizo, sasa itajikita na Somalia pekee.

Akifafanua maslahi ya azimio hilo, Balozi Sellasie amesema, "uamuzi wa Baraza hii leo,  utasaidia kusongesha fursa zote zilizopo sasa za kubadilisha ukanda huo kuwa wa amani na ustawi na kufungua zama mpya ya urafiki baina ya mataifa yote kwenye ukanda huo. Hii itasaidia na kusongesha maslahi ya watu wetu na kuhakikisha maendeleo ya amani na ushirikiano kwenye ukanda huo.”

Hata hivyo Balozi Selassie amesema, "kuondoa vikwazo hivi haimaaninishi ukanda huu umeondokana na changamoto  kwenye ukanda wetu, bado kuna changamoto nyingi ambazo zitahitaji  hatua na dhamira kuzitatua. Bado tunahitaji      msaada mkubwa wa jumuiya ya kimataifa , lakini kwa upande wetu tumejizatiti kuunda ukanda ambao Amani, maendeleo na utulivu vimejikita.

Akizungumza kwenye kikao hicho, mwakilishi wa kudumu wa Eritrea kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Amanuel Giorgio amesema “raia wa Eritrea katu hawatoangalia nyuma, na hawajachukizwa. Huku wakitambua kile walichojifunza katika miongo iliyopita, wameazimia kujenga taifa lenye amani na ustawi ambalo lina thamani ya kujitoa kwao kwa miongo saba ya kujenga taifa lenye maelewano, amani na kujiamini.”

Nchi jirani nazo nazo zilipata fursa ya kutoa maoni ambapo Mwakilishi wa kudumu wa Djibouti kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Mohamed Siad Doualeh, amesema maslahi makuu ya nchi yake ni kupata suluhu ya kudumu na ya amani ya tofauti za mipaka na maeneo kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Amesema “hizo tofauti ziliibuka mwaka 2008 na kusababisha mapigano mwaka  huu, na bado hazijatatuliwa hadi sasa na zinatishia siyo tu Djibouti bali pia amani  na usalama duniani.

Uingereza nayo kupitia mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Karen Pierce amesema, “makubaliano ya kuondoa vikwazo dhidi ya Eritrea yanatambua maendeleo ya amani na  usalama kwenye eneo la pembe ya Afrika sambamba na hatua za Eritrea za kutekeleza matakwa ya Baraza la Usalama. Ni vema kuwa kwa kuzingatia maendeleo hayo, tumezingatia hatua hizi.”

Hata hivyo amesema “ni vema pia tuendelee kuimarisha mazungumzo kati ya Eritrea na Djibouti kuhusu wapiganaji wa Djibouti ambao walipotea vitani sambamba na kumaliza mzozo wa mpaka kati ya nchi mbili hizo.”

Kutokana na Baraza la Usalama kuiondoa Eritrea kwenye vikwazo na kuiacha Somalia pekee kutokana na kuendelea kuzorota kwa hali  ya usalama nchini mwake, mwakilishi wa kudumu wa Somalia kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Abukar Dahir Osman, akafunguka ya kwamba, “vikwazo hivyo dhidi ya Somalia ambavyo vimepitwa na wakati, ni moja ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa vilivyodumu kwa muda mrefu vikigusa maeneo mengi.

Amesema “vikwazo hivyo, siyo  tu vinakiuka umoja wa wasomali bali pia haviendani na sera ya serikali kuu ya Somalia ya kujenga jeshi thabiti la kitaifa.”

Kuondolewa kwa vikwazo ni kilele cha maendeleo ya kisiasa yaliyofuatia kutiwa saini kwa mkataba wa amani kati ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki huko Asmara tarehe 9 Julai mwaka huu.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

Ushirika wenu utaleta amani pembe ya Afrika:Guterres.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amepongeza uhusiano mpya ulioko sasa katika eneo la pembe ya Afrika akisema ni hatua moja muhimu katika kuleta amani kwenye eneo hilo.

Eritrea-Ethiopia asanteni kwa kufungua ukurasa mpya- Baraza la Usalama

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamezipongeza Ethiopia na Eritrea kwa hatua yao ya kutia saini azimio la pamoja la amani na urafiki.