Ushirika wenu utaleta amani pembe ya Afrika:Guterres.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amepongeza uhusiano mpya ulioko sasa katika eneo la pembe ya Afrika akisema ni hatua moja muhimu katika kuleta amani kwenye eneo hilo.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini New York Marekani, Katibu Mkuu amekaribisha zaira ya mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Eritrea, Ethiopia, na Somalia nchini Djibout kuungana na mwenzao wa Djibout, kuwa ni hatua nzuri ya kurejesha uhusiano baina ya mataifa hayo yaliyo katika pembe ya Afrika.
Antonio Guterres amesema makubaliano yaliyofikiwa kati ya mawaziri hao wanne ya kushirikiana ilikurejesha amani na utulivu katika eneo hio ni mfano mzuri wa kuigwa na sehemu zingine.
Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake ikizungumzia ziara hiyo iliyofanyika wiki hii, Guterres amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kuunga mkono mataifa ya eneo la pembe ya Afrika kuimarisha mazuri yaliyopatikana katika kipindi kifupi kilichopita.