Upepo wa matumaini unavuma Afrika- Guterres

16 Septemba 2018

Nchini Saudi Arabia hii leo viongozi wa Rais wa Eritrea Isaias Afwerki  na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed  wametia saini makubaliano ikiwa ni mwendelezo wa hatua kama hiyo iliyofikiwa mwezi Julai mwaka huu na kuzidi kuimarisha azma yao ya kumaliza uhasama uliodumu kwa ya miongo miwili.

Utiaji saini huo umefanyika mjini Jeddah na kushuhudiwa na viongozi kadhaa akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye amesema ni dhahiri shairi kuwa hivi sasa upepo wa amani unavuma barani Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Jeddah hii leo Bwana Guterres amegusia pia makubaliano ya wiki hii kati ya pande kinzani nchini Sudan Kusini ambazo ni serikali na upande unaoongozwa na makamu wa zamani wa rais nchini humo.

Ni kwa mantiki hiyo Bwana Guterres amesema,  “hii ina maana kuwa kuna upepo wa matumaini unavuma barani Afrika, siyo tu kwa amani kati ya Eritrea na Ethiopia bali pia ni ukweli kwamba kesho na keshokutwa hapa Saudi Arabia tutakuwa na maraia wa Djibouti na Eritrea, nchi mbili ambazo zimekuwa mahasimu.”

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa Eritrea na Djibouti nazo zilitangaza Ijumaa kuwa zitarejesha uhusiano wa kidiplomasia kati yao kufuatia kuvunjika kutokana na mzozo wa mpaka mwaka 2008 uliosababisha vifo vya watu kadhaa na kila pande kuteka wafungwa.

UNICEF/Mulugeta Ayene
Afar,Ethiopia mpaka wake na Eritrea

 

Katibu Mkuu Guterres akaenda mbali zaidi akisema kuwa, "nataka niseme kwamba fursa hii ya matumaini ni muhimu mno katika dunia ambayo kwa bahati mbaya matumaini yamekuwa adimu na kwa mara nyingine tena natoa shukrani zangu za dhati kwa serikali ya Saudi Arabia kwa fursa hii ya kushuhudia matukio haya muhimu ambayo hivi karibuni yamesaidia kurejesha tena mazingira ya amani katika dunia yetu iliyosheheni matatizo.”

Katibu Mkuu pamoja na kupongeza serikali ya Saudi Arabia, amepongeza pia Waziri Mkuu wa Ethiopia na Rais wa Eritrea kwa jinsi walivyokabiliana na upinzani wakati wa harakati zao za kusaka kurejesha maelewano kati ya nchi zao.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud