Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani kati ya Eritrea na nchi jirani lazima iende sambamba na kuimarisha haki ndani ya nchi

Sheila Keetharuth, Mtaalam Maalum wa Umoja wa Mataifa  kuhusu haki za binadamu nchini Eritrea.
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Sheila Keetharuth, Mtaalam Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Eritrea.

Amani kati ya Eritrea na nchi jirani lazima iende sambamba na kuimarisha haki ndani ya nchi

Amani na Usalama

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Eritrea, amesema makubaliano ya amani kati ya nchi hiyo na Ethiopia ni lazima yafungue pia nuru ya haki ndani ya nchi hiyo.

Sheila B. Keetharuth amesema hayo leo kupitia taarifa iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi akigusia makubaliano ya amani kati ya nchi hizo yaliyofikiwa mwezi Julai mwaka huu yenye lengo la kumaliza uhasama kati ya pande mbili hizo.

Mtaalamu huyo amesema kinachofanyika kwa lengo la kuleta maelewano ya nje ni lazima kiakisi hali ya ndani ambayo amesema hivi sasa ni tofauti.

Ametoa mfano wa tukio la kukamatwa kwa maafisa 11 wa ngazi za juu wa serikali  ya Eritrea kwa madai ya kukosoa serikali kupitia andiko lao la wazi pamoja na taarifa zinazodai kukamatwa kwa  waziri wa zamani wa fedha ambaye hivi majuzi aliandika vitabu viwili kuhusu hali halisi nchini humo.

Mtaalamu huyo amesema ikiwa taarifa hizo za kukamatwa kwa waziri huyo ni za ukweli, basi zitatoa ishara kuwa kuboreshwa kwa uhusiano wa nchi hiyo na nje si sawa na ilivyo ndani mwa nchi hususan kuhusu  kuheshimu haki za msingi.

Bi Keetharuth amesema ni lazima upatikanaji wa amani kati  ya Eritrea na Ethiopia upongezwe, hata hivyo wakuu wa Eritrea wanapaswa kukumbatia na kutekeleza kwa vitendo hatua madhubuti za kuimarisha  ulinzi na kuheshimu haki za binadamu, sheria na uwajibikaji.