Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Eritrea-Ethiopia asanteni kwa kufungua ukurasa mpya- Baraza la Usalama

Kifaru cha kikosi cha jeshi la kulinda amani Eritrea na Ethiopia UNMEE likishika  doria katika eneo la mpaka kati ya nchi hizo mbili mwaka 2001
UN Photo/Jorge Aramburu
Kifaru cha kikosi cha jeshi la kulinda amani Eritrea na Ethiopia UNMEE likishika doria katika eneo la mpaka kati ya nchi hizo mbili mwaka 2001

Eritrea-Ethiopia asanteni kwa kufungua ukurasa mpya- Baraza la Usalama

Amani na Usalama

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamezipongeza Ethiopia na Eritrea kwa hatua yao ya kutia saini azimio la pamoja la amani na urafiki.

 

Utiaji sahihi wa tamko hilo umefanywa jumatatu kati ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dkt. Abiy Ahmed na Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki mjini Asmara, mji mkuu wa Eritrea.

Katika taarifa yao iliyotolewa leo mjini New York Marekani, wajumbe hao wamekaribisha azma ya pande zote mbili ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na pia kufungua ukurasa mpya  wa ushirikiano.

Pia wamebaini mpango wa vipengele vitano na kufurahia  makubaliano ya kutekeleza uamuzi wa  tume ya mpaka kati ya Ethiopia na Eritrea.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamesema kuwa tukio hili ni la kihistoria na hatua kubwa mbele katika kuleta matumaini katika eneo la pembe ya Afrika na kwingineko.

Katika makubaliano hayo Ethiopia na Eritrea zimekubaliana kwa pamoja  kuhakikisha kuwepo kwa amani katika eneo hilo, maendeleo, ushirikiano na pia Eritrea kuwa mshiriki mkamilifu wa shirika la IGAD.

 

Afar,Ethiopia mpaka wake na Eritrea
UNICEF/Mulugeta Ayene
Afar,Ethiopia mpaka wake na Eritrea

Wajumbe wa Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa wamesema kuwa wako tayari kuzisaidia nchi hizo mbili kutekeleza makubaliano yao na pia kukaribisha  utayari wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia pia katika mchakato wa kuleta amani katika kanda hiyo.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia kuzuru Eritrea na kushangaza wengi kuwa anaunga mkono mpango wa amani ambao umemaliza mvutano wa mpakani uliodumu takribani miongo miwili.

Mataifa hayo yalikuwa yanavutana tangu Ethiopia ikatae uamuzi wa Umoja wa Mataifa na kugoma kuiachia ardhi Eritrea, katika eneo la mpaka kufuatia vita kati yao vilivyoanza mwaka 1998 hadi 2000 ambapo watu 80,000 walifariki dunia.