Hadi sasa hakuna tiba ya UKIMWI: WHO

31 Oktoba 2018

Hadi sasa hakuna tiba dhidi ya Ukimwi na wagonjwa nchini Zimbabwe wanaotumia dawa za kupunguza makali ya virusi vinavyosababisha ugonjwa huo, VVU waendelee kuzitumia.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Harare nchini Zimbabwe na mwakilishi wa shirika la afya duniani WHO nchini  humo, Dkt Alex Gasasira kufuatia taarifa kupitia vyombo vya habari nchini Zimbabwe zinazodai kugunduliwa kwa tiba ya Ukimwi.

Hata hivyo mwakilishi huyo amesema kuwa ARV ambazo ni dawa za kupunguza makali ya VVU zinaweza kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo ili watu wenye VVU, na wale walio hatarini wanaweza kuishi kwa muda mrefu.

UNICEF/Shehzad Noorani
Wanawake wawili walio na VVU wakiwa wamekaa sakafuni wakipokea ARV dawa ya kupunguza makali kutoka kwa muuguzi.

 

“Umoja wa Mataifa unapenda kukumbusha na kuhamasisha watafiti wowote wanaohusika na uendelezaji wa tiba zozote mpya za  magonjwa ikiwemo VVU na UKIMWI kuwasilisha tafiti hizo kwa Wizara ya Afya na huduma za watoto nchini Zimbabwe ili zifanyiwe mchakato wa majaribio ya kitabibu,” amesema Dkt, Gasasira.

Amesema Umoja wa Mataifa  unasisitiza mwongozo wa wizara ya afya katika matumizi ya dawa hizo za kupunguza makali ya UKIMWI na kutaka wagonjwa wote wanaotumia dawa hizo waendelee kuzitumia.

Dkt. Gasarira amenukuliwa akisema kuwa “matumizi ya dawa hizo kwa mujibu wa mwongozo wa kitaifa yamekuwa na matokeo mazuri ya kiafya kwa watu wanaoishi na VVU. Uamuzi wowote wa kusitisha matumizi yake au kubadili ni lazima ufanyike kwa mwongozo wa kina kutoka kwa wahudumu wa afya wenye leseni.”

UN/maktaba
Mhudumu wa afya akiwapatia ushauri nasaha wanawake kuhusu matibabu dhidi ya Virusi Vya UKIMWI, VVU na UKIMWI

 

Wagonjwa wa UKIMWI zaidi ya milioni moja wanapata dawa ya kupunguza makali nchini Zimbabwe,na mpango huo unadhaminiwa na Umoja wa Mataifa, fuko la dunia la kukabiliana na  UKIMWI, Malaria na kifua kikuu; mpango wa dharura  wa rais wa Marekani kuhusu UKIMWI-PEPFAR pamoja na mashirika mengine.

Hatua hiyo imesababisha kupungua kwa vifo vinavyohusiana na UKIMWI kwa asilimia 63 kutoka mwaka wa 2010 hadi 2017.

Umoja wa Mataifa unasadia Zimbabwe kuweza kufanikisha azma yake ya kuutokomeza  UKIMWI ifikapo mwaka wa 2030.

Hadi disemba mwaka wa 2017 asilimia 87 waliokuwa wanaishi na VVU walikuwa wanafahamu hali yao kuhusu VVU ambapo kati  yao hao asilimia 74 walikuwa kwenye matibabu ambapo kati yao kwenye matibabu asilimia 87 walikuwa wanatumia dawa za kupunguza makali.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud