Bado hali ya VVU miongoni mwa watoto na Barubaru Afrika Magharibi na Kati ni mbaya.

Kijana barubaru akifanyiwa vipimo vya Virusi vya UKIMWI huko nchini Ivory Coast
UNICEF/Frank Dejongh
Kijana barubaru akifanyiwa vipimo vya Virusi vya UKIMWI huko nchini Ivory Coast

Bado hali ya VVU miongoni mwa watoto na Barubaru Afrika Magharibi na Kati ni mbaya.

Afya

Katika mkutano wa ngazi ya juu ulioanza leo mjini Dakar Senegal ukiwakutanisha wadau mbalimbali wa afya, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamezisihi nchi za Afrika Magharibi na kati kufanya juhudi zaidi za kuzuia maambukizi mapya ya UKIMWI kwa watoto na barubaru na pia kuongeza upimaji wa Virusi Vya UKIMWI na matibabu. 

Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa ni lile la kupambana na Ukimwi, UNAIDS,  la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la afya, WHO ambapo wito huo wa kuongeza kasi ya kudhibiti maambukizi unazingatia ukweli kwamba mwaka 2017 takribani watoto 67,000 wenye umri wa kuanzia mwaka 0 hadi miaka 9 na barubaru wenye umri wa kuanzia miaka 10 hadi 19 walipata maambukizi mapya ya VVU. 

Theluthi mbili ya idadi hiyo yaani 46,000 ya barubaru waliopata maambukizi mapya ni wasichana.

Taarifa ya UNAIDS inasema kuwa wakati mafanikio yameonekana katika kuzuia maambukizi kwa watoto katika baadhi ya nchi, nchi 11 zikiwa zinaonesha maambukizi kupungua kwa asilimia 35 kati ya mwaka 2010 na 2017, nchi nyingine ikiwemo Nigeria maambukizi katika ukanda huo, ilionekana kutopungua kabisa.

Mkurugenzi mkuu wa UNAIDS Michel Sidibé anasema  nchi za Magharibi na katikati mwa Afrika zina fursa ya kutengeneza mabadiliko chanya kwa watoto na vijana wadogo. Masuala ya msingi ni pamoja na ukosefu wa uwekezaji wa ndani, mifumo tete ya afya, malipo, kukosekana kwa usawa wa kijinsia, unyanyapaa na ubaguzi, hivi vyote  lazima vitizamwe haraka ili ili kuondoa vikwazo na kuokoa maisha.

Katika Afrika Magharibi na Kati, takribani watoto 800 000 na barubaru kwa mwaka 2017 walikuwa wanaishi na Virusi Vya UKIMWI, ikiwa ni idadi kubwa ya pili kote duniani baada ya mashariki na kusini mwa Afrika.