Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zimepigwa lakini safari bado ni ndefu katika vita dhidi ya ukimwi:WHO

 Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Michel Sidibe
Photo: UNAIDS
Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Michel Sidibe

Hatua zimepigwa lakini safari bado ni ndefu katika vita dhidi ya ukimwi:WHO

Afya

Kongamano la 22 la kimataifa kuhusu ukiwmi limefunguliwa rasmi hii leo mjini Amsterdam Uholanzi likihimiza jitihada za kukabiliana na maambukizi mapya hususan kwa vijana barubaru.

Kongamano hilo la siku tano lililoandaliwa na shirika la  afya duniani WHO, lengo lake ni kujadili mustakabali wa ugonjwa wa UKIMWI duniani , kuanzia upimaji hadi matibabu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus ambaye ni  Mkurugenzi  Mkuu wa  WHO, amegusia masuala mbalimbali ikiwemo uvumbuzi wa dawa mpya ya virusi vya UKIMWI au VVU, upimaji wa VVU kwa kutumia vifaa vya kisasa, mbinu mpya za kisasa za ufuatiliaji maendeleo ya waathirika wa VVU duniani na huduma  ya afya kwa wote.Na kuhusu maeneo ambayo bado yanasuasua amesema

(SAUTI YA Dk Tedros Ghebreyesus).

Tunapozungumzia VVU, maeneo ambayo bado yanakabiliwa na changamoto  za maambukizi ni Ulaya Mashariki na Asia ya Kati ambayo ndio maeneo tutakayoyajadili  zaidi katika kongamano hili. Utafiti umebaini kuwa zaidi ya watu theluthi moja wanaishi ya VVU bila kutambua  hali yao kitabibu pia chini ya watu theluthi moja wanaoishi na VVU ndio wanapata dawa za kupunguza makali ya VVU.

Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa pia yanahudhuria kongamano hilo  kama ; shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya UKIMWI  UNAIDS, yamewasilisha ripoti ya pamoja  inayoelezea maendeleo katika mapambano  ya VVU kwa vijana hususan katika kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.

 

Mhudumu wa afya akiwapatia ushauri nasaha wanawake kuhusu matibabu dhidi ya Virusi Vya UKIMWI, VVU na UKIMWI
UN/maktaba
Mhudumu wa afya akiwapatia ushauri nasaha wanawake kuhusu matibabu dhidi ya Virusi Vya UKIMWI, VVU na UKIMWI

Ripoti hiyo iliyopewa jina la “Kwa pamoja kuongeza hatua za mapambano dhidi ya UKIMWI kwa vijana”inatoa mwelekeo wa hatua zilizopigwa katika kanda hiyo kwenye vita dhidi ya maambukizi ya VVU kwa vijana kupitia kampeni, harakati, na uitikiaji wa  vijana katika jitihada zinazofanywa na mashirika hayo katika kukabiliana na tatizo la VVU katika nchini za Afrika Mashariki na Kusini kama Botswana, Swaziland, Ethiopia, Kenya, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Afrika Kusini, Uganda, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Ripoti inasema kumekuwa na mafanikio kwani miaka mitatu tangu kuzinduliwa kwa  mkakati huo wa pamoja , nchini Kenya, vijana barubaru sasa wanatambulika kama kundi muhimu la kufanya nalo kazi katika mapambano na hatua zinazochukuliwa dhidi ya maambukizi ya UKIMWI.

Leila Pakkala ni mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika amesema, wanayo furaha kuzindua ripoti  hiyo ambayo ni jitihada za ushirikiano baina ya mashirika mbalimbali na asasi  za vijana ambapo kwa pamoja waliweza kuzikabili será mbalimbali zinazo  athiri maisha ya vijana wengi.

Naye Catherine Zozi Mkurugenzi wa UNAIDS Afrika Mashiriki na Kusini amesema ripoti hiyo inaonyesha umuhimu wa ushirikiano wenye nguvu na ujumuishwaji wa vijana katika mpango ya kupiga vita UKIMWI.

Mada zingine zinazotamalaki katika kongamano hilo ni pamoja na uvumbuzi wa dawa za kupambana na makali ya VVU.

Meg Doherty ni mtaalamu wa afya wa WHO kuhusu dawa hiyo mpya ya  kupambana na VVU anasema

(SAUTI YA Meg Doherty)

“Kuna dawa mpya ya VVU kwa jina la Dolutegravir ambayo ni moja ya dawa za kupunguza makali ya VVU. Kwa sasa inapatikana kwa ajili ya matumizi kwa waathirika ikijumuishwa na aina zingine mbili za  dawa , na kwa kweli ina nguvu sana katika kupambana na makali ya VVU.”

Na vipi kuhusu ubora na usalama wa dawa hiyo? Bi Doherty amesema

(SAUTI YA Meg Doherty)

WHO imepitisha dawa hiyo, na kutokana na kudhihirika kwa matokeo yake , imeidhinisha matumizi ya dawa hiyo kama moja ya dawa zenye ubora wa juu wa kupambana na VVU.”

Kongamano hilo pia litatoa kipaumbele katika masuala ya ujumuishwaji wa VVU katika huduma  za afya kwa wote , umuhimu wa kufikia idadi kubwa ya waathirika na kushughulikia magonjwa ya VVU yanayoongezeka katika ukanda wa Ulaya ya Mashariki na Asia ya Kati.

Watoto wanne kati ya watano wanaoishi na VVU Afrika Magharibi na Kati bado hawapokei tiba ya kupambana na virusi vya ukimwi. Picha: UNICEF

 

Kongamano hilo litakalokunja jamvi Julai 27 limewaleta pamoja wadau mbalimbali wa afya wa kimataifa, mashirika ya Umoja wa Mataifa , wataalamu wa afya, asasi za kiraia na waathirika wa UKIMWI.