Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 75 ya watu wanaoishi na VVU wanatambua hali zao-  Ripoti

Mandisa Dukashe na familia yake ni wakazi wa Eastern Cape, Afrika Kusini. Mandisa ni muuguzi na anahusika na udhibiti wa VVU na yeye mwenyewe anaishi na VVU. Lakini mumewe na binti zake wamepima VVU na hawana virusi hivyo.
AFP PHOTO/MUJAHID SAFODIEN
Mandisa Dukashe na familia yake ni wakazi wa Eastern Cape, Afrika Kusini. Mandisa ni muuguzi na anahusika na udhibiti wa VVU na yeye mwenyewe anaishi na VVU. Lakini mumewe na binti zake wamepima VVU na hawana virusi hivyo.

Asilimia 75 ya watu wanaoishi na VVU wanatambua hali zao-  Ripoti

Afya

Ripoti mpya kuhusu  hali ya ukimwi duniani imetoa matumaini baada ya kubainika kuwa asilimia 75 ya watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, VVU wanatambua hali zao.

 

Ikipatiwa jina, Ufahamu ni Uthabiti, ripoti hiyo iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na Ukimwi, UNAIDS katika kuelekea siku ya Ukimwi duniani tarehe mosi Disemba, inasema mafanikio hayo yametokana na harakati za kushawishi watu kupima VVU pamoja na kupata matibabu ya kupunguza makali ya virusi.

“Mwaka 2017 asilimia 75 ya watu wenye VVU duniani walifahamu hali zao ikiwa ni nafasi ya juu ikilinganishwa na asilimia 67 mwaka 2015,” imesema ripoti hiyo ikiweka bayana kwa bahati mbaya watu milioni 9.4 wanaoishi na VVU hawafahamu iwapo wana virusi hivyo kwa hiyo hatua ya dharura inatakiwa ili wapatiwe huduma za kupima VVU na matibabu.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kupambamba na Ukimwi, UNAIDS Michel Sidibé amesema hata kama mtu atapima VVU na kupata dawa jambo muhimu ni kuendelea kuchunguza tena na tena kwa miezi 12 mfululizo.

 “Kupima kiwango cha VVU ni kipimo muhimu katika kufuatialia matibabu ya VVU. Inaonekana kuwa tiba inafanya kazi na inasaidia kufuatilia watu ili wawe salama na pia kudhibiti virusi,” amesema Sidibe.

Wanawake wawili walio na VVU wakiwa wamekaa sakafuni wakipokea ARV dawa ya kupunguza makali kutoka kwa muuguzi.
UNICEF/Shehzad Noorani
Wanawake wawili walio na VVU wakiwa wamekaa sakafuni wakipokea ARV dawa ya kupunguza makali kutoka kwa muuguzi.

Hata hivyo ripoti inaonyesha kuwepo kwa utofauti duniani kote katika uchunguzi wa kiwango cha virusi mwilini ambako katika baadhi ya nchi huduma hiyo ni rahisi ikiunganishwa na pale mgonjwa anapokwenda kupata dawa zake, ilhaki katika nchi zingine kuna mashine moja tu nchi nzima kwa ajili ya kupima kiwango cha virusi.

“Kipimo hicho cha kupima virusi kinatakiwa kipatikane Lilongwe Malawi kama ilivyo London, Uingereza,” amesema  akiongeza kuwa “upimaji wa VVU na kiwango cha virusi unapaswa kuwepo kwa ajili ya watu wote wanaoishi na VVU bila tofauti  yoyote.”

Ripoti imetolea mfano huko Côte d’Ivoire, ambako mfuko wa rais wa Marekani wa harakati za kupambamba na Ukimwi, PEPFAR, unasaidia harakati za kitaifa za za kupima virusi vya Ukimwi.

“Katika miaka mitatu tu, kadri idadi ya watu wanaopata matibabu ilivyoongezeka maradufu, maabara 10 za nyongeza za kupima kiwango cha virusi nazo zilianza kufanya kazi. Matokeo yake, huduma ya kupima kiwango cha VVU imeongezeka kutoka asilimia 14 mwaka 2015 hadi asilimia 66 mwaka 2017 na makisio ni kwamba ifikapo mwishoni mwa mwaka huu itakuwa asilimia 75,” imesema ripoti hiyo ambayo imetolewa kuelekea siku ya ukimwi duniani tarehe mosi Disemba, maudhui yakiwa “Ishi kwa matumaini-tambua hali yako ya VVU.

Mtoto mchanga akitolewa sampuli za damu ili apimwe VVU katika moja ya vitu vya kuchunguza Virusi Vya Ukimwi, VVU huko Kyrgyzstan
UNICEF/Aleksei Osipov
Mtoto mchanga akitolewa sampuli za damu ili apimwe VVU katika moja ya vitu vya kuchunguza Virusi Vya Ukimwi, VVU huko Kyrgyzstan


WATOTO NA UPIMAJI WA KIWANGO CHA VVU
 

Ripoti inasema kuwa kwa upande wa watoto, upimaji wa kiwango cha VVU ni muhimu kwa sababu VVU vinashika kasi sana kwa watoto na iwapo amezaliwa na virusi hivyo anaweza kufariki dunia ndani  ya miezi miwili au mitatu.

Hata hivyo changamoto ni mbinu za sasa za kupima VVU kwa mtoto ni hadi pale anapotimu miezi 18 kwa hiyo ripoti inataka mtoto apimwe kiwango cha VVU, huduma ambayo anaweza kufanyiwa ndani ya wiki nne au sita za mwanzo baada ya kuzaliwa.

“Hata hivyo mwaka 2017 ni nusu tu ya watoto waliozaliwa na VVU kwenye nchi zenye mzigo mkubwa wa ugonjwa huo ndio walichunguzwa kiwango cha virusi walipotimiza tu miezi miwili,” imesema ripoti.

VIKWAZO VYA MTU KUTAMBUA IWAPO ANA VVU AU LA

Ripoti hiyo ya UNAIDS inaonyesha kuwa moja ya vikwazo vikubwa vya watu kutambua iwapo wana VVU au la ni ubaguzi na unyanyapaa. Utafiti miongoi mwa wanawake, wanaume, vijana na makundi mengine umebaini kuwa “hofu ya kuonekana kuwa unasaka  huduma za VVU, hofu ya kuwa taarifa hizo zitaenezwa kwa familia, marafiki na wapenzi au jamii nzima huzuia watu kusaka huduma za VVU,ikiwemo uchunguzi.”

Hali ni mbaya zaidi kwa makundi kama vile mashoga, watu waliobadili jinsia, watu wanaotumia madawa ya kulevya, wafungwa na wahamiaji.

Monique (kushoto) amekuwa akienda kila mara katika kituo cha  shirika la EVE for life, linayosaidiwa na UNICEF kuwahudumia watoto na wamama waishio na VVU.
UNICEF/UN0220590/Volpe
Monique (kushoto) amekuwa akienda kila mara katika kituo cha shirika la EVE for life, linayosaidiwa na UNICEF kuwahudumia watoto na wamama waishio na VVU.

MWELEKEO WA HUDUMA ZA UPIMAJI
 

Ripoti inapendekeza kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za upimaji kama vile kwenye jamii, majumbani, huduma ambazo zitasaidia kupunguza vikwazo vya kusaka huduma za VVU.

“Hatuwezi kusubiri watu waugue,” amesema Imam Harouna Koné, Rais wa jukwaa la mitandao ya kupambana na Ukimwi akisema “lazima tuende kwenye jaii na tuwapatie  huduma za kupima VVU na matibabu.”

Ripoti inataka mambo makuu matano kuzingatiwa katika upimaji wa VVU, mambo ambayo yamepatiwa kifupi cha C5 kwa kiingereza.

Mambo hayo ni kuridhia, usiri, ushauri nasaha, matokeo  sahihi ya vipimo na kuunganisha huduma za upimaji na kinga pamoja na matibabu.

“Suala la kwamba mfumo mmoja wa utoaji wa huduma za kupima VVU unaweza kutumika kote ,hilo halipo. Kuna mifumo tofauti na mikakati tofauti ambayo inapaswa kufuatwa ili kufikia watu walio hatarini kupata VVU, ikiwemo mbinu bunifu kama vile mtu kujipima mwenyewe ambapo mtu anakuwa huru zaidi ya kwamba ufaragha wake umeheshimiwa,” amesema .

TAKWIMU ZA VVU/UKIMWI MWAKA 2017
 

Watu milioni 36.9 duniani kote wanaishi na VVU.
Watu milioni 21.7 wanapata huduma dhidi ya VVU
Watu milioni 1.8 wameambukizwa VVU mwaka 2017.
Watu 940,000 wamefariki dunia kutokana na  magonjwa yahusianayo na UKIMWI.