Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi dhidi ya mauaji ya Khashoggi lazima uwe huru: Bachelet

Michelle Bachelet , Kamisha Mkuu  wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa
Picha na UN/Jean-Marc Ferré
Michelle Bachelet , Kamisha Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa

Uchunguzi dhidi ya mauaji ya Khashoggi lazima uwe huru: Bachelet

Haki za binadamu

Kamishina Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu Michelle Bachelet leo amesisitiza tena kwamba mauaji ya mwandishi wa habari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi ni lazima yafanyiwe uchunguzi huru na wa kutoingiliwa, ili kuhakikisha tathimini ya kina na uwajibikaji kwa ukiukwaji wa haki za binadamu uliotekelezwa katika uhalifu huo wa kutisha.

Bi. Bachelet amesema, nakaribisha hatua iliyochukuliwa na uongozi wa Uturuki na Saudi Arabia kuchunguza na kuwafungulia mashitaka washukiwa wa mauaji ya Kashoggi, lakini kwa kuzingatia taarifa kwamba maafisa wa ngazi ya juu nchini Saudi Arabia wamehusika na kwamba mauaji yametokea kwenye ubalozi wa Saudi Arabia,lazima tahadhari iwe ya hali ya juu kuhakikisha uwajibikaji wenye maana na haki dhidi ya uhalifu wa mauaji ya mwandishi huyo wa habari  huyo na mkosoaji mkuu wa serikali.”

Ameongeza kuwa ili uchunguzi huo ufanyike kwa uhuru na bila kuingiliwa na matakwa yoyote ya kisiasa, ushirikishwaji wa wataalamu wa kimataifa ambao watakuwa na fursa ya kupata Ushahidi na kuzungumza na mashahidi ingekuwa bora zaidi.

Bachelet amehimiza kwamba itakuwa muhimu kubaini endapo ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kama utesaji , mauaji na watu kutoweshwa , ulitekelezwa na kubaini wote waliohusika na uhalifu huo bila kujali nyadhifa zao.Kamishina mkuu ametoa wito kwa serikali za Saudi Arabia na Uturuki kutoa ushirikiano katika kuhakikisha kwamba ukweli wa mauaji ya Bwana. Kashoggi unapatikana na pamoja na haki ya kisheria ya familia yake na umma kwa ujumla inatekelezwa.

Kwa mantiki hiyo amesema tathimini ya kitaalamu ikiwemo kuchunguza mwili wa marehemu ni muhimu kwenye uchunguzi wowote wa kesi za mauaji  na hivyo“naitaka serikali ya saudi Arabia kusema wapi ulipo mwili wa marehemu bila kuchelewa kupiga chenga.”