Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saudi Arabia na Uturuki fichueni mnachofahamu kuhusu kupotea kwa Khashoggi- Bachelet

Wandishi wahabari.Hivi karibuni kumeongezeka visa vya kuwatisha, kuwadhalilisha na hata wengine kuuawa.
UN Photo/Violaine Martin
Wandishi wahabari.Hivi karibuni kumeongezeka visa vya kuwatisha, kuwadhalilisha na hata wengine kuuawa.

Saudi Arabia na Uturuki fichueni mnachofahamu kuhusu kupotea kwa Khashoggi- Bachelet

Haki za binadamu

Wiki mbili tangu kutoweka kwa Jamal Khashoggi, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amezihimiza serikali za Saudi Arabia na Uturuki kufichua chochote kile ambacho zinafahamu kuhusu kutoweka au kuuawa kwa mwandishi huyo habari maarufu wa Saudi Arabia, baada ya kutembelea ofisi za ubalozi mdogo wa nchi yake mjini Istanbul.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi, Bi Bachelet, pamoja na kukaribisha hatua ya kukubali wachunguzi kuingia katika ubalozi huo mdogo ili waweze kufanya kazi yao, ameomba pande zote mbili kuhakikisha hakuna vizuizi vyoyote katika uchunguzi wa haraka, kina, fanisi na wa wazi kuhusu kutoweka kwa Bwana Khashoggi.

Ameongeza kuwa, “kwa mujibu wa sheria ya kimataifa, kutoweshwa au mauaji ya kiholela ni uhalifu mkuhbwa na kinga yoyote haipaswi kutumika ili kuzuia uchunguzi wa kile kilichofanyika na nani amewajibika. Wiki mbili ni muda mrefu sana kwa eneo hilo la uhalifu kutokuwa limefanyiwa uchunguzi wa kina wa kimazingira.”

Amesema kwa kuzingatia kuwa kuna ushahidi wa kutosha ya kwamba Bwana Khashoggi  aliingia katika ubalozi huo na tangu hapo hajaonekana tena, ni wajibu wa Saudi Arabia kufichua kile kilichomtokea baada ya kuingia ofisi hizo.

Kamishna huyo Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema Saudi Arabia na Uturuki, ni wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya mateso kwa wanadamu hivyo yanawajibika kuchukua hatua zote kuzuia watu kuteswa, kutoweshwa na vile vile yanapaswa kuchukulia hatua za kisheria wale wote  wanaoshukiwa kufanya vitendo vya aina hiyo.