Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi huru na wa kimataifa ufanyike kuhusu kilichompata Khashoggi- Mtaalamu

David Kaye, mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uendelezaji na ulinzi wa haki za kujieleza na kutoa maoni wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini New Yrok, Marekani tarehe 25 Oktoba 2018
UN /Rick Bajornas
David Kaye, mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uendelezaji na ulinzi wa haki za kujieleza na kutoa maoni wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini New Yrok, Marekani tarehe 25 Oktoba 2018

Uchunguzi huru na wa kimataifa ufanyike kuhusu kilichompata Khashoggi- Mtaalamu

Haki za binadamu

Vuta nikuvute ikiendelea kuhusu kile kilichompata mwandishi wa  habari Jamal Khashoggi kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko Uturuki, hii leo mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ametaka ufanyike uchunguzi wa kina na huru dhidi ya tukio hilo. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

Kilichomkuta Jamal Khashoggi, mwandishi habari mkosoaji wa serikali ya Saudi Arabia, hadi sasa ni kizungumkuti, kila upande yaani Saudi Arabia na Uturuki ikitoa simulizi yake ya kile kilichotokea tarehe pili mwezi huu kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul.

Kutokana na kizungumkuti hicho, mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kutoa maoni na kujieleza David Kaye akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa amesema, “Tumetoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kimataifa kuhusu kutoweka kwa Jamal na hatma ya mauaji yake na kwa kweli nimekatishwa tamaa kuona kuwa wito huu haujatiliwa maanani na nchi husika na ninatoa wito kwa serikali kuitikia siyo tu kwa msingi wa tarehe pili novemba ambayo ni siku ya kukomesha kukwepa sheria kwa vitendo vya uhalifu dhidi ya waandishi wa habari, bali kwa msingi wa tukio la sasa ambapo waandishi wa habari wanakumbwa na shambulio kama hili, wanapaswa kuongeza bidii iwe kupitia Baraza la Usalama, Baraza la Haki za binadamu au kumshawishi Katibu Mkuu afanye hivyo.”

Bwana Kaye amesema wanapaswa kuunda chombo huru cha uchunguzi kiwe na wajumbe watano ambao wanaweza kutathmini taarifa ambazo serikali ya Uturuki imekuwa ikipatia vyombo vya habari na hata kuhoji mashuhuda.

Mtaalamu huyo maalum aamesema jopo hilo linaweza kufanya aina zote za uchunguzi na tathmini na hatimaye kupatia jamii ya kimataifa ripoti sahihi ya kile kilichotokea, “Inaweza isijibu kila swali, lakini itaweza kubainisha nani anawajibika na nini hasa kilitokea na hapo itakuwa ni juu ya jumuiya ya kimataifa kuamua jambo gani la kufanya na taarifa hizo. Lakini nadhani kama hakuna kitu kama hicho, tutaendelea kuwa katika hali ya kutofahamu jambo lipi ni la kweli lipi ni la uongo na tunataka taarifa sahihi ya kile kilichotokea.”