Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bachelet atilia shaka mwenendo wa kesi dhidi ya watuhumiwa wa mauaji ya Khashoggi

Michele Bachelet , Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa , akizungumza na waandishi wa habari 26 Septemba kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York
Picha na UN/Laura Jarriel
Michele Bachelet , Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa , akizungumza na waandishi wa habari 26 Septemba kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York

Bachelet atilia shaka mwenendo wa kesi dhidi ya watuhumiwa wa mauaji ya Khashoggi

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR imesema mwenendo wa kesi dhidi ya watuhumiwa wa mauaji ya mwanahabari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi haukidhi vigezo vilivyotakiwa na Kamishna mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet.

Vigezo hivyo ni kwamba lazima mwenendo wa kesi uwe huru na ukidhi vigezo vya kimataifa ambapo msemaji wa ofisi hiyo, Ravina SHamdasani amethibitisha kuwa wanafahamu ya kwamba kesi hiyo imeanza.

 “Sisi kama unavyofahamu, kwa miezi kadhaa sasa tumekuwa tukishinikiza haki kwa kesi dhidi ya Khashoggi. Tumekuwa tukitoa wito kwa uchunguzi tena uchunguzi huru ukihusisha jopo la kimataifa na hili bado halifanyika,” amesema Bi. Shamdasani.

Ripoti zinasema kwamba, watuhumiwa 11 walifikishwa mahakamani jana Alhamisi kwenye mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh ambapo watano kati yao iwapo watapatikana na hatia ya mauaji ya Khashoggi ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Saudi Arabia, watakabiliwa na adhabu ya kifo.

Khashoggi aliuawa baada ya kutembelea ofisi ndogo ya ubalozi wa nchi yake Saudi Arabia huko Istanbul, Uturuki tarehe 2 mwezi Oktoba mwaka jana.

Bi. Shamdasani amethibitisha kuwa Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwa mara kadhaa amezungumza na mamlaka za Saudi Arabia kuhusu kesi hiyo ya Khashoggi, kabla ya kusisitiza wito wake kwa ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu kuhusu azma  yake ya kutaka kuwepo kwa adhabu ya kifo.

 “Wakati huu ambapo tayari tunafahamu kuwa kesi imeanza huko Saudi Arabia, hii pekee kwanza haitoshelezi na pili tunapinga kuwekwa kwa adhabu ya kifo katika mazingira yoyote yale,” amesema msemaji huyo wa OHCHR huku akiweka bayana kuwa kwa sasa  ofisi yao haina uwakilishi huko Saudi Arabia na hivyo  hawawezi kuwa na tathmini yoyote ya mwenendo wa kesi hiyo.