Chunguzeni kupotea kwa Khashoggi huko Uturuki- Wataalamu UN

9 Oktoba 2018

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameeleza wasiwasi wao mkubwa juu ya taarifa za kutoweka kwa mwandishi wa habari wa Saudi Arabia nchini Uturuki, ambaye hakusita kuikosoa serikali alipohisi inakwenda kombo. 

Jamal Khashoggi ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Saudi Arabia alitoweka punde tu baada ya kuingia katika ubalozi wa nchi hiyo huko Istanbul, Uturuki tarehe 2 mwezi huu wa Oktoba.

Hadi sasa hafahamiki halipo na hakuna mawasiliano yoyote kutoka kwake jambo ambalo limesababisha wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa watoe wito wa kufanyika haraka kwa uchunguzi huru wa kisa hicho.

Wataalamu hao, David Kaye na Agnes Callamard wamenukuliwa katika taarifa iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi wakisema kuwa “Tuna hofu kubwa na kutoweka kwa Khashoggi, na hofu zaidi ni kutokana na madai ya kwamba ni mauaji yaliyokuwa yamefadhiliwa na serikali.”

Kwa mantki hiyo wamesema, “jopo huru la kimataifa lazima lianze kuchunguza kisa hicho. Wahusika au waliopanga mpango huo wawajibishwe. TUnatoa wito kwa serikali ya Uturuki na Saudia Arabia zitoe ushirikiano wa kutosha kwenye kesi hii.”

Wamesema hofu yao ni kwamba kutoweka kwa Bwana Khashoggi kuna uhusiano na kitendo chake cha kukosoa serikali ya Saudi Arabia na sera zake kwa miaka ya hivi karibuni, “tunatoa wito kwa mamlaka za nchi hiyo ziweke wazi fursa za watu kutekeleza haki zao za binadamu ikiwemo haki ya watu kujieleza.

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter