Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IFAD  yapatia wakulima Msumbiji stadi za mapishi bora ili kuepusha utapiamlo kwa watoto

Mtoto mchanga ambaye awali alikuwa amepata matibabu katika kituo cha lishe akipimwa uzito nchini Msumbiji.
©FAO/Eddie Gerald
Mtoto mchanga ambaye awali alikuwa amepata matibabu katika kituo cha lishe akipimwa uzito nchini Msumbiji.

IFAD  yapatia wakulima Msumbiji stadi za mapishi bora ili kuepusha utapiamlo kwa watoto

Afya

Nchini Msumbiji mradi wa Umoja wa Mataifa umewezesha maafisa wa ugani kufundisha wakulima namna ya kulima mazao na kuandaa lishe bora na hivyo kuepusha utapiamlo ambao ni tatizo kubwa kwa watoto hususan kwenye jimbo la Cabo Delgado. 

Katika moja ya viunga vya jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji wakulima wanawake kwa wanaume pamoja na vijana wakiwa shambani wanapatiwa mafunzo kutoka kwa afisa ugani wa kilimo.

Mafunzo haya ni sehemu ya mradi wa mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD wa kuhakikisha wakazi wa eneo hili wanalima mazao  yao kwa bora zaidi na hatimaye waweze kuboresha lishe kwa watoto wao.

IFAD inasema asilimia 43 ya watoto nchini Msumbiji wana utapiamlo na katika jimbo hili la Cado Delgado hali ni mbaya zaidi kwa kuwa kiwango cha utapiamlo miongoni mwa watoto ni asilimia 53.

Baada ya mafunzo wanayopatiwa shambani juu ya ukulima bora, wakulima wakiwa kwenye vikundi wanafundishwa jinsi ya kuandaa chakula bora.

Lucia Lauteno ni mmoja wa wakulima takrbani 5,000 walionufaika na mafunzo hayo ambaye anasema. “nimejifunza maana ya lishe, nimejifunza mambo mengi, mosi ni kuandaa uji ambapo naongezea mayai na mafuta. Watu kwenye jamii yetu wamefurahishwa na kile tunachofanya. Tunapofanya maonyesho yetu ya mapishi baada ya kujifunza wanakuja kuonja  na wanakipenda sana. Kabla ya huu mradi hatukufahamu iwapo kuchanganya vyakula kunaweza kusababisha afya njema . Sasa tuko vizuri na watoto wana nguvu na majirani wanatuuliza watoto tunawalisha nini. “

IFAD inasema kuwa mkulima kama Lucia baada ya kupata utaalamu huo naye anapatia watu wengine katika jamii yake ili kuhakikisha wanaondokana na utapiamlo miongoni mwa watoto mkoani Cabo Delgado.