Skip to main content

Ukame na vita vya Ukraine vimewaacha hoi wakulima nchini Somalia:IFAD

Kituo cha kusambaza maji maeneo yaliyo na ukame Somalia.
© IOM Somalia 2022/ Ismail Osma
Kituo cha kusambaza maji maeneo yaliyo na ukame Somalia.

Ukame na vita vya Ukraine vimewaacha hoi wakulima nchini Somalia:IFAD

Msaada wa Kibinadamu

Mfuko wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo IFAD umeonya kwamba ukame na vita vinavyoendelea nchini Ukraine vimesababisha athari kubwa kwa wakulima nchini Somalia, ambao sasa wanahitaji msaada wa haraka ili kunusuru kilimo na maisha yao kabla hali haijageuka kuwa janga kubwa la kibinadamu. 

Garowe ni moja ya eneo la Somalia lililoathirika vibaya na ukame wa miaka mmne mfululizo. Chakula kimekuwa haba, mifugo haina maji wala malisho na maisha ya wakulima wengi kama Fawzia Salah Mohamud yamesambaratika “Kama wakulima tumeathirika vibaya na ukame , visima tulivyokuwa tukitumia kumwagilia mashamba yetu sasa vyote vimekauka na mashamba yetu yako hatarini kuvamiwa na wanyamapori. Wao pia wameathiriwa na ukame na wanakuja kusaka malisho, pia tumepoteza mazao mengi tuliyotarajia kuyavuna."

Mama akienda kisimani kuteka maji katika kijiji cha Kureyson, Galkayo, Somalia
© UN Photo / Fardosa Hussein
Mama akienda kisimani kuteka maji katika kijiji cha Kureyson, Galkayo, Somalia

Kwa mujibu wa IFAD ukame huu nchini Somalia umesababisha njaa na ugumu wa maisha kwa wakulima, na miezi miwli iliyopita hali imekuwa mbaya zaidi , kwani vita vinavyoendelea nchini Ukraine vimechochea kupanda kwa bei ya mafuta na mbolea kwa asilimia 40, na majanga hayo mawili ukame na vita yamefanya wakulima kupata hasara kubwa kama anavyothibitisha Fawzia Salah “Bei kubwa ya mafuta imetuathiri pia , wakulima wengi hawawezi tena kumudu kununua mafuta na matokeo yake wamepata hasara, Na kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta sasa tunashuhudia athari zake kwa kuongezeka kwa gharama za usafiri, chakula na bidhaa zingine zote muhimu.”

Mbali ya Pembe ya Afrika maeneo mengine yaliyoiathirika vibaya na vita hivyo IFAD inasema ni Sahel, Kusini mwa Afrika, chi za Mashariki ya karibu na Asia ya Kati.

Na kutokana na hali hiyo IFAD imeanzisha mradi maalum kwa kukabiliana na janga hilo wa (CRI) ili kupunguza hatari za kutokuwa na uhakika wa chakula na njaa huku ukilinda maisha ya wakulima wadogo katikia nchi zilizoko hatarini kama anavyosema Donal Brown makamu wa Rais msaidizi wa IFAD "CRI imekuja kuwasaidia kupita kipindi hiki kwa kuwapatia nyongeza ya ruzuku kwa ajili ya kununua mbolea ili kukabiliana na mgogoro huu.”

Shirika hilo pia limetoa wito kwa nchi wanachama kuchangia kiasi kikubwa cha rasilimali ili kuziwezesha nchi 22 zilizoorodheshwa katika mradi huo huku Somalia ilikwa juu kwenye orodha hiyo. Rasilimali hizo zitasaidia wakulima kununua mbolea, mafuta, mbegu na fedha kwa ajili ya upanzi wa msimu ujao.