Janga la kibinadamu likishika kasi Cabo Delgado, UNICEF yafika na kuchukua hatua

27 Oktoba 2020

Katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji, mafuriko yaliyokumba eneo hilo mwishoni mwa mwaka jana na mashambulizi kutoka kwa watu wenye silaha, vimesababisha hali ya kibinadamu kuwa mbaya zaidi na Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la kuhudumia watoto, UNICEF limechukua hatua kuhakikisha linaepusha majanga zaidi ikiwemo kusambaa kwa ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Mkuu wa mawasilino wa UNICEF nchini Msumbiji, Daniel Timme amezuru eneo hilo hivi karibuni ambapo amesuhudia siyo tu hali halisi lakini vile vile hatua zinazochukuliwa na shirika hilo kuboresha maisha ya binadamu.

Bwana Timme ambaye alitembelea kijiji kidogo cha Impire kwenye jimbo la Cabo Delgado lililoko kaskazini kabisa mwa Msumbiji amesema hali ya kibinadamu inazidi kuzorota kila uchao. Kimbunga na mafuriko! Lakini kubwa zaidi hivi sasa ni mashambulizi kutoka kwa wanamgambo waliojihami ambayo yamesababisha watu kukimbilia maeneo ya kusini ya jimbo la Cabo Delgado.

Vurugu zinatokea katika maeneo ambayo tayari yalikuwa na matatizo mengine kama Cabo Delgado ambako tayari kulikuwa kumekumbwa na matatizo ya mafuriko na umaskini
UN Mozambique
Vurugu zinatokea katika maeneo ambayo tayari yalikuwa na matatizo mengine kama Cabo Delgado ambako tayari kulikuwa kumekumbwa na matatizo ya mafuriko na umaskini

“Zaidi ya watu 200,000 jimboni Cabo Delgado wamekimbia ghasia na wengi wao wanaishi kwenye maeneo ya malazi yenye msongamano kama kwenye ua huu wa shule ya trés de fevereiro. " amesema Bwana Timme akiongeza kuwa  wakimbizi hao wengine wanaishi na familia wenyeji na bila shaka mahitaji  ni pamoja na chakula na malazi, huduma za matibabu.

ameongeza kuwa, “Ni muhimu sana kuzingatia viwango vya afya na kuepuka kusambaa kwa COVID-19 na magonjwa mengine kama kipindupindu. Ni kwa sababu hiyo tumefunga katika kambi yote hapa vituo vya watu kuna mikono kwa maji na sabuni ili kuepusha kuenea kwa magonjwa.”

Kutokana na COVID-19, UNICEF inaunda vikosi vya kupeleka huduma vijijini na kwa wakimbizi badala ya kujenga vituo vya afya na zaidi ya yote kuhusu maji safi ya kunywa kwa hiyo, “ni muhimu pia watu wawe na maji safi na salama ya kunywa. Na kwa sababu hiyo tunafunga mabomba ambako watu watapata maji ya kunywa na pia ya kujisafi.”

Hivi karibuni shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR liliripoti kuwa kutokana na mashambulizi huko Cabo Delgado, raia zaidi ya 1,000 wamevuka mto Ruvuma na kuingia Tanzania.
 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter