Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Familia zilizoathirika na machafuko Cabo Delgado Msumbiji zapata fursa ya kuanza upya maisha: FAO

Baada ya kulazimika kutoroka nyumbani kwake katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji, Ali Ndalila aliweza kuanzisha upya maisha yake kwa msaada wa FAO na washirika wake.
©FAO/Fábio de Sousa
Baada ya kulazimika kutoroka nyumbani kwake katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji, Ali Ndalila aliweza kuanzisha upya maisha yake kwa msaada wa FAO na washirika wake.

Familia zilizoathirika na machafuko Cabo Delgado Msumbiji zapata fursa ya kuanza upya maisha: FAO

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO limeanzisha mradi ambao unatoa matumaini mapya ya maisha kwa wakimbizi wa ndani nchini Msumbiji.

Wakati Ali Ndalila alipolazimika kukimbia nyumbani kwake katika jimbo la kaskazini mwa Msumbiji la Cabo Delgado, aliumia moyoni kwa sababu nyingi ikiwemo kulazimika kuacha mavuno yao mengi ambayo yalitokana na msimu mzuri na wa bahati wa mvua.

Eneo hilo limebarikiwa kuwa na mandhari ya kuvutia, kuanzia fukwe za bahari ya Hindi hadi milima mizuri ya ajabu, lakini maisha ya amani ya wakazi milioni 2.3 wa eneo hilo yamesambaratishwa katika kipindi cha miaka sita iliyopita na ghasia kutoka kwa makundi yasiyo ya serikali.

Ali, mkewe Florinda na watoto wao watano ni miongoni mwa watu zaidi ya milioni moja ambao wamefurushwa kutoka kwenye makazi yao, na ambao sasa wanategemea msaada kutoka shirika la FAO na washirika wake kuwasaidia kuanza upya maisha yao.

Viongozi wa vijiji walimpa Ali shamba na FAO ilimpatia vifaa vya kilimo, ikiwa ni pamoja na mbegu za mboga na zana, ili aweze kuanzisha tena kilimo ili aweze kulisha familia yake.
©FAO/Fábio de Sousa
Viongozi wa vijiji walimpa Ali shamba na FAO ilimpatia vifaa vya kilimo, ikiwa ni pamoja na mbegu za mboga na zana, ili aweze kuanzisha tena kilimo ili aweze kulisha familia yake.

Kutokana na kuweza kujikimu kwa kulima mahindi na mbaazi kwenye shamba lake la ekari mbili katika kijiji cha Namande, familia ya Ali haikuwa na chaguo ila kuacha kila kitu nyuma wakati waasi waliposhambulia kijiji chao, wakiteketeza nyumba nyingi. Walielekea wilaya ya jirani ya Montepuez na kufika "tukiwa na shukrani kwa ajili ya maisha yetu lakini tukiwa tumekata tamaa kwa mustakabali wetu na nini kingetokea kwetu," Ali analalamika.

Mahitaji yao ya haraka yalitimizwa na binamu wa Ali ambaye anaishi huko na ambaye aliwachukua na kuwalisha, bado Ali alihuzunika kushuhudia shinikizo kubwa kwa binamu yake wa kuhitaji kuzisaidia kaya hizo mbili.

Kusaidia familia zilizotawanywa

Mamlaka ya eneo hivi karibuni ilimgawia Ali na familia yake shamba la nusu ekari kwa ajili ya kulima.

Kisha FAO ikampatia vifaa vya ukulima ili kumwezesha kurejea katika uzalishaji. Kama ilivyo kwa wakimbizi wengine wa ndani au IDPs, Ali alipokea mbegu za mboga za kutosha na zana za kilimo kutoka FAO ili kuzalisha chakula cha kutosha kwa familia yake kwa muda wa miezi sita.

Msaada huo, unaotolewa chini ya mpango wa kukabiliana na mafanikio ya kilimo wa kaskazini mwa Msumbiji unaoendeshwa na FAO, ambao unasaidiawakimbizi wa ndani na jumuiya za wenyeji kwa zana na mafunzo ya kuongeza na kubadilisha mapato yao, kupata chakula bora na kuboresha mlo wao.

Zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Cabo Delgado ni wakulima wadogo wanaotegemea kilimo kwa ajili ya kuendesha maisha yao, kwa hivyo, ghasia na migogoro katika eneo hilo zimeathiri sana, sio tu usalama na ustawi wao, lakini pia maisha na lishe yao.

Wakati inapiga jeki wakimbizi wa ndani, FAO pia inaunga mkono jamii zinazowakaribisha kuhimiza ushirikishwaji wa kijamii, kujenga mazingira ya amani na kupunguza shinikizo za maliasili.

Ali anayejivunia mazao bora aliyoweza kuzalisha, kuuza ziada ili aweze kununua mahitaji kama vile dawa.
©FAO/Fábio de Sousa
Ali anayejivunia mazao bora aliyoweza kuzalisha, kuuza ziada ili aweze kununua mahitaji kama vile dawa.

Fursa ya kuanza upya maisha

Ali anasema usaidizi aliopokea umempa fursa ya maisha mapya "Ardhi, mbegu, pembejeo na usaidizi wa kiufundi vyote vimechangia kwa kiasi kikubwa hadi mahali nilipo leo," anasema kwa hisia.

Sasa anaweza kulisha kaya yake kwa raha na kuuza mazao ya ziada ili kununua mahitaji mengine kama vile dawa.

"Tayari nimeanza kuuza mazao kutoka katika shamba langu jipya," Ali anasema, na kuongeza kuwa, "vitunguu na kabichi vinapata bei nzuri kwa sababu ubora ni wa kiwango cha juu kuliko chaguzi zinazopatikana sokoni."

Ali pia amepata msaada wa kiufundi kuhusu zao la bamia, maboga na maharage kutoka kwa maafisa ugani wa FAO, ambao mara kwa mara hurudi kuangalia maendeleo yaliyofanywa na washiriki wa mradi huo.

Kwa Ali, pamoja na kumbukumbu zake nzuri kwa majina na nyuso zao maafisa ugani hao, wamekuwa watu wanaofahamika ambao anafurahi kukutana nao tena.

"Pamoja na washirika wetu wa serikali za mitaa, FAO imekuwa ikileta mabadiliko katika maisha ya wakimbizi wenfi wa ndani kama Ali na familia yake, lakini kiwango cha wakimbizi wa ndani wakati wa ghasia huko Cabo Delgado kinaendelea kutishia maisha ya familia zaidi na hasa mahitaji. Kuongezeka kwa jitihada zetu za kusaidia jamii zinazowakaribisha nawakimbizi wa ndani wanaporejea katika mazingira wasiyoyafahamu,” anasema mwakilishi wa FAO nchini Msumbiji, Dario Cipolla.

Mazao ya mboga utoka shamba la Ali
©FAO/Fábio de Sousa
Mazao ya mboga utoka shamba la Ali

Ali ni dhibitisho lililo hai kwambawakimbizi wa ndani wanaweza kujipatia usaidizi unaofaa ambao unawasaidia kuzalisha riziki na kujumuika kwa urahisi zaidi katika jamii zinazowakaribisha.

Huku mzozo huo ukisababisha zaidi ya watu milioni moja waliokimbia makazi yao hadi sasa na uwezekano wa watu wengi zaidi kuhama, FAO na washirika wake wa ndani wanatoa wito kwa nchi kutoa msaada zaidi ili shirika liendelee kusaidia zaidi ya wakimbizi wa ndani 967,000 katika 2023.