Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujasiri wa Indonesia baada ya tsunami na tetemeko la ardhi ni wa kipekee- Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akikagua uharibifu katika hospitali ya Anutapura huko Palu kwenye kisiwa cha Sulawesi nchini Indonesia hii leo 12 Oktoba 2018, kufuatia tetemeko la ardhi lililokumba kisiwa hicho tarehe 28 mwezi Septemba mwaka huu
OCHA/Anthony Burke

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyeko ziarani nchini Indonesia, leo ametembelea eneo la Sulawesi lililokumbwa na tetemeko la ardhi na tsunami tarehe 28 mwezi uliopita wa Septemba.

Bwana Guterres amepita katika fukwe ya Talise na kutembelea hospitali ya Balaroa ambayo iliharibiwa kwa kiasi kidogo wakati wa tetemeko la ardhi wiki mbili zilizopita lakini bado inaendelea kuhudumia wagonjwa.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Balaroa baada ya kutembelea maeneo hayo Katibu Mkuu amesema ni vigumu sana kutovunjika moyo pindi mtu anaposhuhudia kile alichokiona, lakini “ni wakati wa kuelezea kuwa nataka, kwa niaba ya Umoja wa Mataifa na jamii nzima ya kimataifa kuonyesha mshikamano wetu na wananchi wa Sulawesi na wa Indonesia kwa  ujumla na jinsi ambavyo tunavutiwa na mnepo wao baada ya tetemeko hili.”

Leo tarehe 12 Oktoba 2018, Katibu Mkuu wa UN António Guterres ametembelea kambi inayohifadhi wakimbizi wa ndani waliokumbwa na tetemeko la ardhi na tsunami huko Sulawesi, Indonesia. Huduma kambini zinatolewa na shirika la kiraia la kitaifa na UNFPA

Bwana Guterres amesema ujasiri wao na ari yao ya mshikamano ni ya kipekee, akiongeza kuwa “napenda kutoa shukrani zangu kwa kasi na ufanisi ulioonyeshwa na serikali ya Indonesia.”

Katibu Mkuu amesema kuwa “sisi Umoja wa Mataifa tuko tayari kusaidia serikali, tayari tuna wetu kwenye eneo husika. Lakini jukumu la kuongoza jitihada hizi linapaswa kuwa la serikali na jamii ya kimataifa iunge mkono juhudi hizo. Na ndio sababu ya uwepo wetu na ahadi yetu thabiti kwa watu wa Sulawesi na watu wa Indonesia na kuvutiwa kwetu na kile kinachofanyika hapa.”

Tetemeko la ardhi na Tsunami vilikumba Indonesia tarehe 28 mwezi Septemba mwaka huu ambapo hadi sasa zaidi ya 2,000, wamefariki dunia huku watu takribani 200,000 wameathiriwa na zahma hiyo.