Sasa naweza hata kubadili nguo kwa faragha- Mnufaika wa mahema ya UNHCR

Mfanyakazi wa UNHCR akimfariji manusura wa tetemeko la ardhi na tsunami nchini Indonesia.
UNHCR/Fauzan Ijazah
Mfanyakazi wa UNHCR akimfariji manusura wa tetemeko la ardhi na tsunami nchini Indonesia.

Sasa naweza hata kubadili nguo kwa faragha- Mnufaika wa mahema ya UNHCR

Msaada wa Kibinadamu

Mgao wa mahema kwa manusura wa tetemeko la ardhi na  tsunami huko Indonesia umeanza kuleta matumaini kwa familia ambazo zililazimika kuishi kwenye makazi ya muda yasiyo na utu.

Mgao  huo kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR umewezesha watu 10,000 wakiwemo wanawake na watoto angalau kuweza kuendelea na maisha yao, ingawa si katika makazi yao waliyokuwa wamezoea.

Miongoni mwao ni Bampek mwenye  umri wa miaka 45 pamoja na mkewe na watoto 8 ambaye anasema, “wakati mwingine mvua iliponyesha, maji yaliingia kutoka kila pembe lakini sasa zahma hiyo imesalia historia.”

UNHCR baada ya kusambaza mahema hayo, wadau wa ndani na nje wa Indonesia walisaidia kuyafunga kwa uimaria na hatimaye kukabidhi kwa wananchi  hao ambapo msaada mwingine ambao shirika hilo linepelekea wananchi  hao ni pamoja na mikeka ya kulalia, vyandarua vya kuzuia mbu na kandili za sola.

Vemy ambaye ni mkewe Bampek akikagua makazi yao mapya anasema “nafurahi kwamba sasa nina amani. Jinsi ambavyo kuna mgao ndani ya  hili hema, mimi na watoto wangu wa kike tunaweza kubadilisha nguo zetu kwa faragha.”

Mnufaika mwingine ni Titin mwenye  umri wa miaka 34, kwake yeye  mahema haya yamemuokoa na madhila yaliyompata baada ya tetemeko ardhi mwezi uliopita kwa kuwa alisalia bila makazi. “Sifahamu ningalikuwa wapi hivi sasa kama si kwa msaada wa hema lenu,” Titin amewaeleza wafanyakazi wa UNHCR.

Kwa mujibu wa ofisi ya kitaifa ay kushughulikia majanga nchini Indonesia, tetemeko hilo la ardhi lililofuatiwa na tsunami limeharibu nyumba 68,000 na kuanza watu 200,000 bila makazi na zaidi ya 2,000 walipoteza  maisha.

UNHCR inashirikiana na wadau wake kusaidia serikali ya Indonesia ili kukidhi mahitaji ya kibinadamu  yanayoongezeka kila uchao ambapo hadi  leo  hii mahema 2,000 ya familia yamesambazwa na makaratasi 12,400 ya nailoni yamesafirishwa kwa ndege hadi Sulawesi ya Kati tangu wiki iliyopita.