Ni lazima kila liwezekanalo lifanywe kukabili mabadiliko ya tabia nchi:Guterres

Mtu akitembea na kuona gari linaloning'inia kwenye paa ya nyumba baada ya tetemeko la ardhi na tsunami Palu katikati ya Sulawesi Inonesia 29 Septemba 2018
© UNICEF/Arimacs Wilander
Mtu akitembea na kuona gari linaloning'inia kwenye paa ya nyumba baada ya tetemeko la ardhi na tsunami Palu katikati ya Sulawesi Inonesia 29 Septemba 2018

Ni lazima kila liwezekanalo lifanywe kukabili mabadiliko ya tabia nchi:Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa serikali za nchi za Kusini na Mashariki mwa asia kushika usukani katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi na athari zake.

Wito huo ameutoa leo mjini Bali Indonesia katika mkutano wa viongozi wa jumuiya ya nchi za Kusini na Mashariki mwa Asia , ASEAN.

Akitoa salamu za rambirambi na mshikamano na waathirika wa tetemeko la ardhi na tsunami lililoikumba Indonesia hivi majuzi amesema nchi nne zinazoathirika Zaidi na majanga hayo ni wanachama wa ASEAN ambazo ni Myanmar, Thailand, Ufilipino na Viet Nam.

Amerejelea haja ya utekelezaji wa mpango wa pamoja wa ASEAN na Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabia nchi ambao ni muelekeo wa hatua mbalimbali za utekelezaji wa ajenda ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu SDG’s ifikapo mwaka 2030. Pamoja na kuupongeza ukanda huo kuwa umepiga hatua ya kiuchumi kwa nusu karne iliyopita na kupunguza umasikini bado inakibarua kigumu katika masuala mawili aliyoyatilia msisitizo katika hotuba yake ambayo ni, “Mosi changamoto ya kutokuwepo usawa , napongeza juhudi zenu za kupunguza pengo la maendeleo miongoni mwa nchi za ASEAN, lakini kukomesha kutokuwepo usawa ni lazima tuchukue mikakati mbalimbali kutokomeza umasikini na maendeleo jumuishi, hii ikimaanisha kuboresha elimu kwa wote , kuboresha mifumo ya kodi ili kuweza kukusanya mapato Zaidi kwa ajili ya maendeleo endelevu.”

Rio Saputra, mwenye umri wa miaka 10 akiwa mbele ya nyumba yao iliyosambaratishwa kwa tsunami huko eneo la Sulawesi Kati nchini Indonesia. (Picha ya tarehe 3 Oktoba)
UNICEF/UN0240792/Wilander
Rio Saputra, mwenye umri wa miaka 10 akiwa mbele ya nyumba yao iliyosambaratishwa kwa tsunami huko eneo la Sulawesi Kati nchini Indonesia. (Picha ya tarehe 3 Oktoba)

Na akaongezea kwamba “Suala la pili muhimu ninalotaka kujikita nalo ni mabadiliko ya tabia nchi  , ASEAN inalitambua hili vyema kabisa , kama mabadiliko ya tabia nchi yanakwenda kasi kuliko sisi basi wakati umetutupa mkono, lakini vado hatujachelewa tunaweza kudhibiti ongezeko la joto na kusalia nyuzi joto 1.5

Guterres ametaja mifano ya hatua za kuchukua ikiwa ni pamoja na kuacha kukata misitu, kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya mafuta yenye hewa ukaa nyingi, na kujikita katika nishati mbadala , kilimo kinachojali mazingira na utafiti wa tekinolojia mpya  zitakazosaidia kulinda mazingira na kupunguza hewa ukaa.

Na kisha akawaambia akawageukia viongozi wa dunia akiwakumbusha kuhusu mkutano wa Desemba COP24 utakaopanyika Poland“Nawatolea wito wa kufanya kila muwezalo kutatua masuala muhimu na kuhakikisha dunia inaondoka Katowice Poland na muongozi madhubuti wa utekelezaji wa mkataba wa Paris kwani hili ni la lazima.”

Guterres kesho Ijumaa atasafiri kwenda mjini Palu  katikati ya jimbo la Sulawesi ili kujionea athari za tsunami na tetemeko la ardhi lililotokea mwishoni mwa Septemba.