Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rwanda, Kenya na Côte d’Ivoire kidedea ripoti ya Benki ya Dunia

Kilimo barani Afrika kinapaswa kuangaziwa upya ili kisiwe chanzo cha kudorora kwa uchumi
FAO/Alessandro Stelzer
Kilimo barani Afrika kinapaswa kuangaziwa upya ili kisiwe chanzo cha kudorora kwa uchumi

Rwanda, Kenya na Côte d’Ivoire kidedea ripoti ya Benki ya Dunia

Ukuaji wa Kiuchumi

Kasi ya  ukuaji uchumi kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ni ndogo kuliko ilivyotarajiwa, imesema ripoti mpya ya Benki ya Dunia kwa mwezi huu wa Oktoba. Siraj Kalyango na ripoti kamili.

Ripoti hiyo inayotolewa mara mbili kwa mwaka imesema wastati wa ukuaji uchumi unakadiriwa kuwa asilimia 2.7, ikiwa ni ongezeko kidogo sana kutoka asilimia 2.3 mwaka jana.

Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia kwa kanda ya Afrika Albert Zeufack amesema mwelekeo huu wa kusuasua ni kiashiria kuwa mazingira ya nje hayako rafiki kwa ukuaji wa uchumi wa Afrika.

Mathalani mwelekeo wa biashara duniani umeyumba, bei za mazao na chuma zimeporomoka kutokana na hofu juu ya masuala ya ushuru.

Halikadhalika bei ya chuma nayo inaweza kuporomoka zaidi mwaka 2019 kutokana na kupungua kwa mahitaji hususan nchini China.

Hata hivyo ripoti inasema kwa Kenya, Rwanda na Côte d’Ivoire, uchumi umesalia thabiti kutokana na uzalishaji imara kwenye kilimo na sekta ya huduma sambamba na kuongezeka kwa uwezekaji wa umma.

Ripoti imesema hatua za nchi hizo tatu zimeinua kipato cha wananchi ambao wamekuwa na  uwezo wa kununua huduma na bidhaa.

Habari si  nzuri kwa Nigeria, Angola na Afrika Kusini kwa kuwa ripoti inasema uchumi haukukua kutokana na anguko la uzalishaji wa mafuta kwa Nigeria na Afrika Kusini huku sababu ya kudorora kwa Afrika Kusini ikiwa ni kusinyaa kwa sekta ya kilimo.

Bwana Zeufack anasema muarobaini wa kudorora kwa uchumi kwa  nchi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara ni watunga será wajikite zaidi kwenye uwekezaji wa kuboresha uwezo wa nguvukazi, wapunguze uelekezaji wa fedha kwenye sekta zisizo na tija na pia waangazie maeneo ambayo yatawezesha kupunguza kukua kwa deni la taifa.