Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za Afrika zapokea mitaji mingi isiyo rasmi kuliko ilivyodhaniwa- IMF

Kakao ni moja ya mazao ya kibiashara kutoka barani Afrika
UNDP Guatemala/Caroline Trutmann
Kakao ni moja ya mazao ya kibiashara kutoka barani Afrika

Nchi za Afrika zapokea mitaji mingi isiyo rasmi kuliko ilivyodhaniwa- IMF

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti mpya ya shirika la fedha duniani, IMF iliweka bayana juu ya ongezeko la mitaji huko Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara na hii leo mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo anaweka bayana kile kilichovutia wawekezaji.

Kiwango cha mitaji isiyo rasmi inayopelekwa katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara kimeongezeka kutoka dola bilioni 4  mwaka 1980-1990  hadi dola bilioni 25 mwaka 2007 na kuongezeka zaidi ya maradufu hadi dola bilioni 60 mwaka 2017.

Naibu Mkuu wa idara ya Afrika ndani ya IMF Mahvash Saeed Quresh ambaye ni mwandishi wa ripoti ya hivi karibuni zaidi  ya shirika hilo kuhusu mtazamo wa uchumi kwenye eneo hilo ametaja sababu za ongezeko hilo kuwa ni pamoja na zile za kimataifa akisema, "katika kusaka mapato, pindi kiwango cha riba nchini Marekani kinapokuwa cha chini, watu wanasaka kuwekeza kwenye maeneo ambako kiwango cha riba kipo juu. Sababu nyingine ni kuepuka hasara ambayo hii hupimwa na kuwepo kwa masoko yasiyotabirika, vipimo vya masoko yasiyotabirika, na tatu ni bei za bidhaa, ambapo  bei zinaposonga, wawekezaji wanapata fedha zaidi na hivyo kuwa na fedha za kuwekeza.Lakini pia upande wa ndani, nchi nyingi za Afrika zilizo kusini mwa Sahara ni wauzaji wa bidhaa nje kwa hiyo zinakuwa na uchumi mzuri kwa hiyo zinapokea fedha nyingi.”

Bi. Quresh amefafanua kuwa wawekezaji wengi wa ndani katika nchi hizo za Afrika ni wale wasio raia ambao pindi wakishuhudia hali  ya kiuchumi inayumba wanaelekeza mitaji maeneo mengine.

Hata hivyo amesema ni dhahiri kuwa nchi za Afrika zimekuwa zikipokea kiwango kikubwa cha mitaji kuliko nchi zinazoibuka kiuchumi.