Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukuaji wa kiuchumi Afrika ni chini ya makadirio ya awali- Benki ya Dunia

Makonteina katika bandari moja yakionyesha kuimarika kwa uchumi
Photo: Dominic Sansoni/World Bank
Makonteina katika bandari moja yakionyesha kuimarika kwa uchumi

Ukuaji wa kiuchumi Afrika ni chini ya makadirio ya awali- Benki ya Dunia

Ukuaji wa Kiuchumi

Katika ripoti iliyotolewa hivi karibuni, Benki ya Dunia imesema ukuaji wa uchumi kusini mwa jangwa la Sahara umepungua mwaka 2019 kufuatia kutotabirika kwa hali ya kiuchumi duniani na kasi ndogo ya mabadiliko ndani ya nchi.

Toleo la 20 la Benki ya Dunia linaloangazia hali ya kiuchumi kwenye bara la Afrika, PULSEl linasema kwa ujumla ukuaji wa uchumi kwenye eneo hilo unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia2.6 mwaka huu wa 2019 kutoka asilimia 2.5 mwaka 2018, ambayo ni asilimia 0.2 chini ya makadirio ya mwezi Aprili.

Albert Zeufack, Mchumi Mkuu wa Afrika kwenye Benki ya Dunia amesema, “ukuaji hafifu unaashiria mambo matatu, kwanza ongezeko la uhasama wa biashara unaoathiri dunia nzima, sio tu Afrika. Pili kasi ndogo ya mabadiliko ndani ya nchi hususan, namna ya kukabiliana na deni na utendaji wa taasisi katika sekta ya umma. Tatu, athari za mabadiliko ya tabianchi kwa mfano vimbunga vilivyoathiri, Msumbiji, Zimbabwe na Malawi mapema mwaka huu na ukame na mafuriko ambavyo vinaathiri uzalishaji kote Afrika.”

 Amesema “hayo yote yanachangia katika kupungua kwa viwango vya mauzo nje ya nchi na uwekezaji katika nchi za Afrika. Kwa njia moja, serikali, taasisi na watu binafsi hawako katika sehemu ya kuendelea kubuni ajira ambazo zinahitajika sana.”

Nigeria, Angola, Afrika Kusini zasuasua

Nje ya kusini mwa jangwa la Sahara, Benki ya Dunia imesema taswira iko tofauti tofauti. Mathalani, harakati za kujikwamua kiuchumi kwa mataifa ya Nigeria,Afrika Kusini na Angola, ambayo ndiyo yenye uchumi thabiti zaidi barani Afrika, zimesalia dhaifu na kuathiri ukuaji uchumi kwenye ukanda wa Afrika.

Nchini Nigeria, ukuaji katika sekta zisizo za mafuta umesalia kuwa mdogo, huku Angola sekta ya mafuta imesalia kuwa dhaifu huku huko Afrika Kusini, uwekezaji mdogo unaathiri shughuli za kiuchumi.

Kando na nchi hizo tatu, Benki ya Dunia imesema ukuaji katika maeneo mengine ya bara hilo unatarajiwa kusalia kuwa na kasi, ingawa unatarajiwa kupungua katika baadhi ya nchi.

Kwa wastani ukuaji katika nchi zisizo na raslimali za asili unatarajiwa kushuka, hii ikiashiria athari za vimbunga nchini Msumbiji na Zimbabwe, hali ya sintofahamu ya kisiasa nchini Sudan, kupungua kwa mauzo ya nje nchini Kenya na hatua za serikali nchini Senegal kupunguza madeni na mapungufu ya bajeti.

Benki ya Dunia imesema mataifa manne kati ya 10 au watu takriban milioni 146 waliishi kwa kiwango cha chini ya dola 1.90 za kimarekani kwa siku mwaka 2015.

Fursa finyu za kiuchumi na kupunguza hatari kwa watu maskini, umaskini uliokithiri vitakuwa sehemu ya maisha ya waafrika kufikia mwaka 2030. Kwa mujibu wa ripoti ajenda ya umasikini inahitaji kuweka watu masikini katika usukani na kusaidia kuimarisha mabadiliko, kutumia fursa ya mifumo ya vyakula nje na ndani ya mashamba, kukabiliana na hatari na mizozo na kutoa fursa bora na zaidi kwa ajili ya fedha kwa umaa kuimarisha maisha ya watu walioko hatarini zaidi.

Sehemu muhimu itakuwa katika kukabiliana na pengo la huduma za kiafya, kielimu, uwezeshaji na ajira.

Wanawake kupiku wanaume kwenye ujasiriamali Afrika

Wafanyabiashara wanawake Tanzania wamesaidia kukuza kiwango cha uchumi kutokana na harakati zinazoendelea za usawa kijinsia.
Picha na UNCTAD
Wafanyabiashara wanawake Tanzania wamesaidia kukuza kiwango cha uchumi kutokana na harakati zinazoendelea za usawa kijinsia.

 Benki ya Dunia pia imesema ni katika ukanda wa Afrika tu duniani ambako kuna uwezekano wa wanawake wengi kuwa wajasiriamali kuliko wanaume na kuchangia takriban asilimia 40 ya nguvu kazi kwenye sekta ya kilimo barani kote. Hata hivyo kuna pengo kubwa katika uzalishaji na malipo ambavyo vinahitaji kushugulikiwa.

Mchumi mkuu huyo wa Afrika kwenye Benki ya Dunia amesema kuna suluhu mbali mbali za kupunguza umasikini na kuimarisha uwezo wa wanawake akisema kwamba, “nchi za Afrika zinahitaji kuelimisha wasichana wake, hususan wasichana wenye umri mdogo, kuhakikisha wanakwenda shule muda mrefu na kuwapatia stadi ambazo wanahitaji kwa ajili ya kufanya kazi. Hii itachangia katika kupunguza mimba za utotoni na kuimarisha vipato na kuongeza umri wa kuolewa.”

Aidha ameongeza kwamba nchi za Afrika zinahitaji kuwekeza katika miundombinu inayokabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuweka será kwa ajili ya kuzuia hatari na majanga ya asili akiongeza kwamba, “majanga ya asili yanaathiri vibaya watu masikini na wanawake.”


 

TAGS: Benki ya dunia, uchumi, Afrika