Awamu ya pili ya majadiliano ya kuunda serikali mpya Sudan Kusini yamefanyika mjini Juba

12 Septemba 2019

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na aliyekuwa naibu wake Riek Machar wamekamilisha majadiliano ya siku ya pili mjini Juba nchini Sudan Kusini huku viongozi hao wawili wakirejelea azma ya kufikia amani huku wakiahidi kukutana mara kwa mara kuelekea uundaji wa serikali ya mpya ya umoja wa kitaifa inayotarajiwa Novemba 12 mwaka huu 2019.

Mkutano huo ambao ulimfikisha kiongozi wa upinzani Riek Machar aliyekuwa anasubiriwa, ulisheheni sala, nyimbo na maombi.

Taswira hii ikishabihiana na tukio la mnamo Aprili mwaka huu ambapo katika ziara yao huko Roma Italia viongozi hao wa Sudan Kusini walikutana na Papa mtakatifu na katika kitendo kilichozua hisia alibusu miguu ya viongozi hao wawili kama ishara ya kunyenyekea kuwasihi kuungana kuleta amni nchini humo.

Miongoni mwa waliohudhuria ni Askofu Alkangelo Wani Lemi, mwenyekiti wa baraza la makanisa nchini Sudan Kusini

(Sauti ya Askofu Lemi)

« Licha ya ukubwa wa changamoto ambazo zitatukabili, ni jukumu letu kufanya lile ambalo ni sahihi, na hilo ni kuja pamoja na kutafakari, ni katika kutafakari, na majadiliano na kuketi kwa pamoja na kukubaliana, na kuweka kil kitu mezani, na tuyajadili kwa ajili ya watu ambao mikono yao haijawasamehe viongozi wao. »

Baada ya mkutano wa faragha wawakilishi wa viongozi hao wawili walizungumza na waandishi wa habari, ambapo msahuri maalum wa maswala ya usalama na mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya uundaji wa serikali ya mpito Tut Gathluak amesema

(Sauti ya Tut)

“Pande husika za makubaliano ya amani wamekuwa mjini Juba kasoro Riek na sasa kwa sababu Riek ameungana na timu hii inamaanisha kwamba pande zote za makubaliano ya amani wapo hapa Juba. Hii ni hatua njema na dhamira kuelekea utulivu nchini Sudan Kusini

Kwa upande wake naibu mwenyekiti wa kikundi cha upinzani  cha SPLM-io nchini Sudan Kusini Henry Odwa amesema 

(Sauti ya Henry)

“Tumejadili pia kuhusu pande ambazo hazikutia saini mkataba, kama mnavyofahamu kuna vyama ambavyo vinaongozwa na Thomas Cirilo na Paul Malong na ni muhimu kuwashirikisha. Bila wao mchakato wa amani huenda ukakabiliwa na changamoto na hiyo ndio sababu ni lazima tusonge kwa pamoja kama watu wa Sudan Kusini. »

Kando na mahitaji ya kufadhili mchakato wa amani, sehemu ya majadiliano ilisisitiza umuhimu wa kupeleka ujumbe wa amani katika kila sehemu ya Sudan Kusini na kwingineko.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter