Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Kiir na Machar umerejesha imani Sudan Kusini- Deng Gai

Taban Deng Gai, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa New York, Marekani 26, Septemba 2019.
UN /Laura Jarriel
Taban Deng Gai, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa New York, Marekani 26, Septemba 2019.

Mkutano wa Kiir na Machar umerejesha imani Sudan Kusini- Deng Gai

Amani na Usalama

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo limejulishwa kuwa mkutano kati ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na mpizani wake Riek Machar kwenye mji mkuu Juba hivi karibuni ulikuwa ni fursa pekee ya kutatua masuala muhimu ambayo hayajapatiwa ufumbuzi kwenye mzozo unaoendelea nchini humo.
 

Makamu wa kwanza wa Rais wa Sudan Kusini Taban Deng Gai amesema  hayo leo mjini New York, Marekani wakati akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74.

Bwana Deng Gai amesema, “hatua hiyo itafungua njia ya kuundwa kwa serikali mpya ya kitaifa nchini Sudan Kusini ifikapo tarehe 12 mwezi Novemba mwaka huu wa 2019.”

Bwana Deng Gai amesema ziara hiyo ya Bwana Machar ilikuwa ni ya kihistoria na imeleta imani iliyokuwa inahitajika zaidi miongoni mwa viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na raia wa Sudan Kusini.

Makamu huyo wa kwanza wa rais amerejelea kuwa mwaka jana watu wengi wasiokuwa na matumaini waliona Sudan Kusini iko kwenye hatihati ya kutumbukia kwenye vita na walikuwa na hofu iwapo mkataba wa amani utazingatiwa au la.
 

“Hivi sasa Sudan Kusini inaelekea kwenye zama za amani na utulivu wa kudumu,” amesema Bwana Deng Gai.

Makamu huyo wa kwanza wa Rais nchini Sudan Kusini amesema tangu kutiwa saini kwa mkataba mpya wa amani ulioboreshwa, “kwa ujumla hali ya usalama Sudan Kusini imekuwa tulivu.Serikali na pande husika kwenye mkataba wamekuwa wakishirikiana kwa umakini ndani ya mifumo tofauti iliyowekwa na kamati ya kutekeleza kipindi cha mpito Sudan Kusini iliyoanzishwa kusimamia vipengele vya mkataba huo.”

Mapigano yaliyoanza nchini Sudan Kusini mwezi Desemba mwaka 2013 yalisababisha mamia ya maelfu ya raia wa nchi hiyo kukimbia makazi yao na kusaka hifadhi maeneo mengine ya nchi hiyo au nchi jirani.