Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baadhi ya maduka ya nyama yafungwa Harare ili kuepusha kuenea Kipindupindu

Iwapo usafi hautazingatiwa katika maduka ya nyama kuna hatari kubwa ya kuenea zaidi kwa kipindupindu, na serikali  ya Zimbabwe imechukua hatua
AMISOM/Omar Abdisalan
Iwapo usafi hautazingatiwa katika maduka ya nyama kuna hatari kubwa ya kuenea zaidi kwa kipindupindu, na serikali ya Zimbabwe imechukua hatua

Baadhi ya maduka ya nyama yafungwa Harare ili kuepusha kuenea Kipindupindu

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO linaimarisha juhudi zake za kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu nchini Zimbabwe wakati huu ambapo ugonjwa huo unaenea kasi kwenye mji mkuu Harare wenye zaidi ya watu milioni mbili.

Mlipuko huo ulianza tarehe mosi mwezi huu na hadi tarehe leo takribani watu 4000 walikuwa wanashukiwa kuwa na ugonjwa huo, na tayari watu 25 wamefariki dunia.

WHO inasema kitovu cha mlipuko ni kitongoji cha Glenview mjini Harare na sababu kuu ni ukosefu wa huduma za  maji safi na salama, hali inayosababisha wakazi wake kutumia maji ya visima.

Msemaji wa WHO mjini Geneva, Uswisi, Christian Lindmeier akizungumza na waandishi wa habari hii leo amesema tayari serikali ya Zimbabwe imetangaza hali ya dharura wakati huu ambapo maambukizi mapya kila siku ni kati ya watu 400 hadi 700 na kwamba…

(Sauti  ya  Christian Lindmeier)

“Kama sehemu ya hali ya dharura, serikali imefunga baadhi ya shule na kupiga marufuku uuzaji wa nyama katika maeneo yaliyoathirika. Halikadhalika serikali imeanza kukarabati mabomba ya majitaka na kuongeza usambazaji wa maji majumbani kwenye maeneo yaliyo na maji yasiyo salama.”

Na kwa upande wake WHO tayari ina wataalamu wake Harare ambao wanasaidia siyo tu kwenye utoaji wa chanjo dhidi ya kipindupindu bali pia kuelimisha jamii jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo.

Kipindupindu ni ugonjwa unaoenezwa kwa kunywa maji machafu hususan  yenye kinyesi na unazuilika hata hivyo unaweza kusababisha kifo ndani ya saa chache iwapo mgonjwa hatatibiwa.

Zimbabwe imekuwa ikikabiliwa na milipuko ya kipindupindu mara kwa mara na mlipuko mkubwa zaidi ni ule wa kuanzia mwezi Agosti 2008 hadi Mei 2009 ambapo ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 4000.