Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko India kwa kampeni yenu ya kutokomeza kujisaida hovyo hadharani- UN

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kati) katika mkutano wa kimataifa wa Mahatma Gandhi uliofanyika leo huko New Delhi India ukiangazia huduma za kujisafi.
UN in India/Vishal Singh
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kati) katika mkutano wa kimataifa wa Mahatma Gandhi uliofanyika leo huko New Delhi India ukiangazia huduma za kujisafi.

Heko India kwa kampeni yenu ya kutokomeza kujisaida hovyo hadharani- UN

Afya

Kampeni ya India ya kuhakikisha kuwa inaweka maeneo yake safi na kuondokana na tabia iliyokuwa imeota mizizi ya kujisaidia hovyo hadharani imepigiwa chepuo hii leo na Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyeko ziarani nchini India.

Alikuwa akizungumza mjini New Delhi  wakati wa tukio maalum la kumkumbuka baba wa Taifa hilo, Mahatma Ghandi lilioenda samamba na mkutano wa siku nne wa kujadili ajenda ya kujisafi ifikapo  mwaka 20130, suala ambapo hayati Gandhi alipigia kampeni.

“Napongeza India kwa kulipatia kipaumbele cha  juu suala la kuondoka na kujisaidia hadharani, ikiwa kipaumbele cha serikali nzima na napongeza serikali za majimbo ambazo zimeridhia mipango na kutenga bajeti ya kutokomeza kitendo cha kujisaidia hadharani," amesema Bwana Guterres.

Kampeni ya India Safi ilianza mwaka 2014 ikilenga kusafisha mitaa, barabara, miundombinu katika majiji, miji na maeneo ya vijijini ili kuwa na India safi ifikapo  mwaka 2019.

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kati) kwenye mkutaon wa kimataifa wa huduma za kujisafi uliofanyika New  Delhi India leo ikiwa ni sehemu ya kumkumbuka baba wa taifa hilo, Mahatma Gandhi
UN India/Vishal Singh
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kati) kwenye mkutaon wa kimataifa wa huduma za kujisafi uliofanyika New Delhi India leo ikiwa ni sehemu ya kumkumbuka baba wa taifa hilo, Mahatma Gandhi

Katibu Mkuu akasema kuwa huduma duni za kujisafi husababisha magonjwa, watu kukosa faragha na pia kupoteza utu na zaidi ya yote huchochea ukosefu wa usawa kati ya wanawake na wanaume, masikini  na matajiri, miji na vijijini na kwamba lina athari kubwa katika haki za binadamu na utu wa kibinadamu. “Huduma duni za kujisafi na kujisaidia haja kubwa hadharani vina athari mbaya sana kwa wanawake na wasichana. Wanaweza kukabiliwa na unyanyasaji zaidi, uhuru wao binafsi kudhibitiwa n ahata wanashindwa kutembea hapa na pale na bila kusahau athari za kiafya kwa sababu wanakosa huduma za kujisafi na vifaa vya hedhi.”

Katibu Mkuu akakumbusha kuwa ajenda 2030 inaweka bayana matarajio ya kuhakikisha kila mtu anakuwa na huduma za kujisafi anazohitaji na kwamba India itakuwa imefikia malengo  hayo kabla ya mwaka, ikijumuisha “wanawake, watoto, vijana na watu wenye ulemavu, wazee na watu wa jamii ya asili, na wale wasio na makazi, wafungwa, wakimbizi na wahamiaji,”

Hata hivyo amesema baadhi ya makundi hayo ni vigumu kuyafikia na kinachotakiwa ni mbinu bunifu, ujasiri na uongozi thabiti kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.

“Ninajivunia na nina furaha kuwepo hapa katika tukio hili muhimu. Nashukuru serikali ya India kwa kuwa wenyeji wetu na ninawapongeza tena na tena kwa maendeleo mliyofikia, Umoja wa Mataifa uko tayari kuwasaidi,” amesema Katibu Mkuu akisema kwamba hatua iliyochukuliwa na India ni kiashiria jinsi utashi wa kisiasa unavyoweza kuleta mabadiliko na kufanikisha ajenda yenye matarajio makubwa.