Bado nchi nyingi haziwekezi kwenye mifumo ya maji safi- Ripoti

28 Agosti 2019

Shirika la Afya Duniani WHO na kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachoratibu masuala ya maji, UN-Water wametaka hatua za dharura zaidi za kuwekeza kwenye huduma za maji safi na salama pamoja na mifumo ya huduma za kujisafi. 

Wito huo unakuja wakati idara za kimataifa za maji zinakutana mjini Stockholm kwenye mkutano wake wa kila mwaka wakati wa wiki ya maji duniani kati ya tarehe 25 na 30 Agosti mwaka 2019.

Hii ni kufuatia ripoti mpya iliyochapishwa na WHO kwa niaba ya UN-Water iliyofichua kuwa mifumo dhaifu ya serikali na kutokuwepo na ufadhili inahujumu upatikanaji wa na huduma za usafi katika nchi maskini duniani.

“Watu wengi sana hawapati maji safi ya kunywa, huduma za kujisafi hali inayowaweka katika hatari ya maambukizi  na pia kuhujumu maendeleo katika sekta ya afya ya umma, amesema Dkt.  Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.

Utafiti kuhusu maji safi na salama uliofanyika mwaka huu katika mataifa  115 ukijumuisha watu bilioni 4.5 umeonesha udhaifu katika ufadhili na uwekezaji kwenye sekta ya maji.

Nchi 19 ziliripoti kasoro ya asilimia 60 ya ufadhili ilhali ni chini ya asilimia 15 ya nchi zilizo na fedha zinazoweza kufadhili mipango yao.

Hata hivyo ripoti hiyo imebani kuwa uwepo wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs hususan namba 6 umesaidia kuimarisha huduma za maji safi na kujisafi.

Takribani asilimia 50 ya nchi zilizofanyiwa utafiti kwa sasa zimeweka malengo ya maji safi na salama ya kunywa yanayolenga kufikia viwango vya juu ifikapo mwaka 2030, kwa mfano kutatua suala la ubora wa maji na kuongeza upatikanaji wa maji kwenye makazi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud