Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viwavi jeshi sasa vyaingia Asia, mazao hatarini - FAO

Shamba la mahindi lililoshambuliwa na viwavi jeshi Malawi. Sasa vyahamia Bara Hindi.
FAO/Rachel Nandalenga
Shamba la mahindi lililoshambuliwa na viwavi jeshi Malawi. Sasa vyahamia Bara Hindi.

Viwavi jeshi sasa vyaingia Asia, mazao hatarini - FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Viwavi jeshi vinaweza kutishia uhakika wa chakula na maisha ya mamilioni ya wakulima wadogo barani Asia wakati huu ambapo wadudu hao waharibifu wanahofiwa kuwa wataeneza zaidi kutoka India huku maeneo ya kusini-mashariki mwa Asia na kusini mwa China kuwa hatarini zaidi.

Limeonya shirika shirika la chakula na kilimo duniani FAO katika taarifa yake iliyotolewa leo huko Roma Italia na Bangkok, Thailand.

FAO inasema kuwa wadudu hao walionekana hivi karibuni nchini India, ikiwa ni mara ya kwanza barani Asia.

“Wadudu hao wana uwezo wa kusafiri umbali wa kilometa 100 kwa usiku mmoja,” imesema taarifa hiyo ya FAO ikiongeza kuwa wanaharibu mimea yote kwa mwaka mzima kwa kuzingatia hali nzuri ya hewa ya ukanda huo ya kitropiki, ikimaanisha kuwa kuna mazao na magugu kila wakati ambayo ni chakula cha viwavi hao.

Mkurugenzi Mkuu msaidizi wa FAO ambaye pia ni mwakilishi wa shirika hilo kanda ya Asia na Pasifiki, Kundhavi Kadiresan, amesema kuwa wadudu hao wanaweza kuleta balaa kwa wakulima wa mahindi na mpunga na hivyo kuathiri mbinu yao ya kujipatia kipato.

Ili kukabiliana na tishio hilo FAO imetoa mapendekezo ambayo yamekuwa na mafanikio makubwa katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.

Mapendekezo hayo ni pamoja na kutumia vyema dawa za kuua wadudu, kufuatilia mwenendeo wa wadudu hao na kutoa onyo mapema, kutumia mwongozo wa wakulma na wafanyakazi wa ugani ambao unaelimisha juu ya kukabiliana na viwavi  jeshi hao.

Wakulima wadogo wadogo barani Asia  hulima  takriban asilimia 80 ya eneo la bara hilo na kupanda mahindi na mpunga, mazao ambayo ni nafaka muhimu kwa chakula.