Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Apu ya Nuru kumkomboa mkulima Afrika- FAO

Viwavi jeshi katika  mmea wa mahindi Lesotho
FAO/Lesotho/Lechoko Noko
Viwavi jeshi katika mmea wa mahindi Lesotho

Apu ya Nuru kumkomboa mkulima Afrika- FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Apu iliyopatiwa jina la Nuru na ambayo inazungumza lugha tatu; Kiswahili, Kifaransa na Twi  imezinduliwa na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO kwa lengo la kuwezesha mkulima kubaini aina mpya ya viwavijeshi ambavyo ni tishio kwa mazao barani Afrika. 

Apu hiyo Nuru ya kukabiliana na viwavi jeshi imeanzishwa kwa ushirikiano kati ya FAO na Chuo Kikuu cha jimbo la Pennsylvania cha nchini Marekani.

Aina hiyo mpya ya viwavi jeshi ilionekana kwenye nchi za Afrika Magharibi mwaka 2016 na mwaka 2017 ikaenea kwa kasi kubwa kwenye nchi zote za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara .

Wadudu hao waharibifu wa mazao walishambulia mamilioni ya eka za mahindi na kutishia uhakika wa chakula kwa zaidi ya watu milioni 300.

FAO inasema wakulima wengi wanaweza kuwa wamesikia kuhusu mdudu huyo lakini ndio wanamuona kwa mara ya kwanza hivyo wasitambue ni jambo gani la kufanya.

Kwa mantiki hiyo Nuru inaleta nuru kama anavyoelezea Allan Hruska, afisa kutoka FAO.

(SAUTI YA ALLAN HRUSKA)

 “ Nuru ni msaidizi mpya wa kidigitali atakayetoa ushauri kwa wakulima wa jinsi ya kukabiliana na viwaji jeshi katika mataifa yaliyo chini ya jangwa la Sahara barani Afrika. Kwa hivyo atazungumza kwa wakulima katika lugha zao, kwa sasa anajua lugha tatu/Nne  lakini atajifunza zingine nyingi kupitia mashine. Ataelewa maswali ya wakulima watakayomuuliza naye kujibu maswali hayo katika lugha zao”

FAO inasema apu hiyo itasaidia wakulima kutambua adui wao mpya na hivyo kuchukua hatua kuweza kumuua. 

Naye Profesa kutoka Chuo Kikuu cha Pennsylvania, David Hughes, ambaye ameongoza kutengeneza apu hiyo amefananisha “Nuru” na afisa ughani ambaye kila wakati yuko na wakulima mashambani mwao.