Wenye bahati Yemen hula mlo mmoja kwa siku- OCHA

3 Agosti 2018

Nchini Yemen hali ya kibinadamu hususan upatikanaji wa chakula inazidi kuwa ya shida kila uchao kwa wananchi ambapo Umoja wa Mataifa unasema wale wenye bahati angalau wanaweza kula mlo mmoja kwa siku, ilhali idadi kubwa wanakula mara chache kwa wiki.

Mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini Yemen, Lise Grande akihojiwa kwa njia ya simu na Idhaa ya kiarabu ya Umoja wa Mataifa kutoka mji mkuu Sana’a amesema kwa sasa watu milioni 8.5 nchini humo wanakabiliwa na njaa kali akisema..

 (Sauti ya Lise Grande)

“Unajua uhalisia wa familia hizi ni kwamba kama wana bahati wanaweza kula mlo mmoja kwa siku. Idadi kubwa ya watu milioni 8.5 wenye njaa wanakula mlo mmoja baada ya siku mbili na familia nyingi angalau zinakula mara cahche kwa wiki. Unajua hili ni janga ambalo limesababishwa na hii vita.”

Bi. Grande amesema hali ya sasa ya mkwamo wa upatikanaji wa chakula ikiendelea, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu watu wengine milioni 10 watakuwa hawana chakula na hivyo idadi kuongezeka hadi milioni 18.5.

Kwa mantiki hiyo amesema..

(Sauti ya Lise Grande)

“Ni wakati wa pande husika kukomesha chuki, kukomesha vita na kusaka njia ya kusonga mbele na kusaka suluhu ya kisasa. Gharama ya vita hii imekuwa ni kubwa sana, mamilioni ya maisha yako mashakani. Wakati umefika ikome.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter